Namibia kuongozwa na mwanamke? | Mwananchi

Windhoek. Chama tawala cha Namibia, Swapo, kinaendelea kuongoza katika kura zinazoendelea kuhesabiwa kufuatia uchaguzi wa urais na Bunge uliofanyika Jumatano iliyopita Novemba 27.

Mgombea kupitia tiketi ya Swapo, Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajiwa kuibuka mshindi kutokana na kuongoza katika kura.

Hadi sasa Tume ya Uchaguzi ya Namibia (ECN) imeonesha Nandi-Ndaitwah anaongoza kwa kura za urais kwa asilimia 54.82, huku asilimia 65.57 ya kura zote zikiwa tayari zimehesabiwa.

Chama cha Swapo kilichoiongoza Namibia tangu uhuru wake kutoka kwa utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini mwaka 1990, kilimteua Ndaitwah ambaye ni makamu wa Rais kuwa mgombea wake wa urais.

Uchaguzi huo uliofanyika Novemba 27, 2024 ulisogezwa hadi Novemba 30 katika vituo kadhaa baada ya baadhi ya watu kushindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na matatizo ya kiufundi na uhaba wa karatasi za kupigia kura.

Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini Namibia, mgombea wa urais anatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote ili kushinda moja kwa moja.

Iwapo hakuna mgombea anayefikia asilimia hiyo, duru ya pili ya uchaguzi itahitajika ili kumpata mshindi wa mwisho.

Mpinzani wake wa karibu, Panduleni Itula wa chama cha upinzani cha Independent Patriots for Change (IPC), alikuwa na asilimia 28.09 ya kura za urais.

Awali, IPC ilikuwa na matumaini ya kuumaliza utawala wa miaka 34 wa Chama cha Swapo.

Iwapo Nandi-Ndaitwah ataendelea kuongoza hadi matokeo ya mwisho, atakuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini humo na mmoja wa viongozi wachache wa kike barani Afrika.

Related Posts