Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, amezungumza na DW na kueleza mkasa mzima wa jinsi watekaji hao walivyomkamata na kumtesa mnamo Desemba Mosi mwaka huu saa 10 alfajiri.
“Wakanifunga wakaniningiza juu juu, wakapitisha chuma mguu kwa mguu, halafu pingu wakaweka kwa chini, halafu chuma wakaningiza kwa juu, haalfu kwa hiyomi nikawa naninginia. Huku wakiendelea kunipuga, Nimepata maumivu, kwa sababu walikuwa wananipiga na gongo,” alieleza Nondo.
Kwa mujibu wa Nondo baada ya tukio hilo, watekaji hao walimtupa eneo la ufukwe wa Coco Beach, ambako anaeleza alichukua usafiri wa pikipiki hadi ofisi za ACT na baadaye alikimbizwa hospitali ya Aga KHAN.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi, Tanzania lilitoa taarifa na kueleza kuwa linafanya uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kujua sababu ya Nondo kutekwa ili hatua za kisheria zichukuliwe. Kutokana na namna tukio hilo lilivyokuwa, ACT Wazalendo jana walitoa tamko wakilihoji jeshi la polisi maswali Matano, kuhusu kutekwa kwa Nondo.
Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Rukaiya Nassir, ACT walitaka majibu kutoka kwa jeshi la polisi. Na baadhi ya maswali yao yalikuwa, Je pingu zilizoanguka na kuokotwa wakati Nondo akikamatwa zilikuwa za nani? wakalihoji jeshi hilo zaidi, iwapo wamebaini polisi waliohusika kumteka, kumpiga na kumtelekeza Mwenyekiti wao.
Baada ya mkasa wa Nondo ACT yaliomba Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi kwa raia
Hata hivyo kuhusu gari, Jeshi la polisi kadhalika lilitoa ufafanuzi kuwa liliegeshwa katika kituo hicho cha polisi cha Gogoni tangu Novemba 29 na kwamba lilitolewa Desemba 1 kwa ajili ya Kwenda kuoshwa.
Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo Dorothy Semu, amezungumza na kutoa msimamo wa chama kuhusu tukio hilo la kutekwa na kuteswa kwa Nondo.
“Tunalitaka jeshi la polisi lisimamie weledi wake, lisimamie majukumu yake, litekeleze kazi yake ya ulinzi wa rai na mali zao, lituambie ni nani hao wanaosimamia, wanaoamrisha, utakumbuka si Abdul Nondo aliyepitia utekaji huu wapo wengine wengi,”alieleta Dorothy Sema.
Wachambuzi wa masuala ya siasa hapa nchini wamekuwa na mtazamo kuhusu utekaji huo. Mwanadiplomasia na mchambuzi wa masuala ya siasa Tanzania, Deus Kibamba amesema kuna shida kubwa juu ya ulinzi wa haki ya kuishi.
”Kwa moyo, macho, masikio na ulimi wangu, nakemea na kulaani kabisa kabisa kabisa vitendo vya utekaji kama ambavyo Abdul Nondo na wengine, utekaji ni hatua ya kwanza ya mtu kuondolewa uhai wake,” alisema Kibamba.
Nondo anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana alfajiri ya Desemba Mosi, akiwa kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli iliyoko Mbezi Louis, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.