Mbeya. Wakati Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Mbeya likisema watembea kwa miguu, abiria na bodaboda ni chanzo cha ajali za mara kwa mara barabarani, limetangaza msiamo mpya wa kukabiliana na changamoto hiyo.
Akizungumza leo Jumanne Desemba 3, 2024 wakati wa utoaji elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, Notker Kilewa amesema abiria na watembea kwa miguu wamekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani.
Amesema kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka, hawataruhusu magari mabovu kufanya kazi yoyote akiwaomba wananchi kufichua vyombo vyote ambavyo havina sifa.
“Wengine ni wasomi lakini hawafuati sheria za barabarani, madereva wanakosa uvumilivu, ndio maana tumeanza na elimu kwa taasisi ya elimu hasa kwa shule za msingi, sekondari na vyuo,” amesema kamanda huyo.
Amesema abiria wengi ambao ni wafanyabiashara kwa kutaka kuwahi kwenye biashara zao, humchochea dereva akimbize gari na matokeo yake huwa ni ajali.
Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani mkoani Mbeya, Rajabu Ghuliku amesema wameamua kuwafikia wanafunzi kwa kuwa ndio viongozi na mabalozi wa baadaye.
Amesema kutokana na makundi hayo kuishi katika mikusanyiko, wanaamini elimu hiyo itawafikia watu wengi zaidi na kuondokana na ajali za mara kwa mara.
“Tunapoelimisha wanafunzi hawa 600 tunaifikia jamii kubwa, tumeanza na Mbeya Day, Chuo Kikuu Katoliki (CUoM) na tutahitimisha na Shule ya Msingi Imezu,” amesema Ghuliku.
Mwanafunzi Alinanuswe Kassim wa CUoM, amesema elimu hiyo imewafungua akili ya kuanza kuzingatia sheria na alama za barabarani akiahidi kuwa balozi kwa wenzake.
“Ni sahihi tumekuwa tukivuka maeneo kama za mataa na zebra tukichati na simu au kusikiliza miziki, lakini kwa elimu hii lazima tuitumie vyema kwa usalama wetu,” amesema Alinanuswe.
Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Imezu, Jesca Mwampashi ameshauri elimu hiyo kuwa endelevu bila kujali kalenda na matukio ya usalama barabarani ndiyo inatolewa.
“Hata sisi wanafunzi tunafarijika kuona askari na viongozi wengine wakubwa wakitutembelea kutupa elimu juu ya maisha yetu, tunaomba iwe endelevu,” amesema Mwampashi.