Rais Samia: Mifumo ya utoaji haki muhimu kwa ukuaji uchumi EAC

Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa mifumo ya utoaji haki na usimamizi wa sheria katika kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia jijini Arusha leo Jumanne Desemba 3, 2024, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mifumo hiyo ni msingi wa utawala wa sheria, uhuru wa mahakama na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akihutubia katika kongamano la 21 la mwaka la Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA), Majaliwa amesema mifumo madhubuti ya utoaji haki inasaidia ujumuishaji wa kikanda na kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Mfumo ulioimarishwa wa utoaji haki ni muhimu kwa ujumuishaji wa kina wa kikanda na ukuaji wa uchumi. Kongamani hili ni muhimu kwa kuwa sasa litatoa fursa ya kushughulikia changamoto zinazotukabili na kupanga mikakati ya kuzitatua,” amesema.

Akizungumzia changamoto za uhalifu wa kimataifa wa kupangwa, Majaliwa amesema unadhoofisha mifumo ya haki, usalama wa umma na utulivu wa kiuchumi. Hivyo, amesema kuna haja ya kuongeza juhudi za kikanda katika kushughulikia uhalifu huo kwa mikakati shirikishi.

“Kadri eneo letu linavyozidi kuunganishwa kupitia biashara na uhamaji wa wafanyakazi, tunakuwa hatarini zaidi kwa uhalifu wa kimataifa. Ni muhimu tuunde mifumo jumuishi inayozingatia utawala wa sheria na haki za binadamu,” amesema.

Hata hivyo, amesema tayari kunahatua zilizopigwa na Tanzania katika kuboresha utoaji haki kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

“Mahakama ya Tanzania imeimarika kupitia Tehama, hatua inayowezesha haki kufikiwa kwa urahisi. Serikali itaendelea kuiunga mkono mahakama kuhakikisha haki inapatikana kwa ufanisi,” amesema Majaliwa.

Kauli za viongozi wengine

Rais wa EAMJA, Jaji John Keitirima akizungumza katika kongamano hilo, amesema linakusudia kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa kushirikiana kikanda na kukuza hatua zitakazochangia uboreshaji wa uzingatiaji wa sheria na uhuru wa mahakama.

Rais huyo amesema jukwaa hilo ni muhimu kwa kubadilishana ujuzi na uzoefu ili kuboresha huduma za mahakama katika EAC.

Mapema, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Mahakama ni kitovu cha amani na haki na amewataka majaji na mahakimu kuendelea kulinda uaminifu wa wananchi kwa mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema juhudi za kuimarisha mahakama za kitaifa zitasaidia ukuaji wa uchumi na ushirikiano wa kikanda.

Hivyo, ametoa rai kwa vyama vya majaji na mahakimu kutafuta fedha za kuwasaidia mahakimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu, ili wapate mafunzo na maarifa mapya.

Jaji mkuu huyo amesemalengo ni kutaka  kuimarisha utawala wa sheria na mifumo ya haki kwa masilahi ya ukanda mzima wa EAC.

Kongamano hilo linaongozwa na kaulimbiu isemayo; ‘Kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa ushirikiano wa kikanda na ukuaji wa uchumi.’

Related Posts