Saba wafariki dunia, tisa majeruhi ajali iliyohusisha lori, Hiace na Costa

Kagera. Watu saba wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa katikia ajali iliyohusisha lori la mizigo aina ya Scania, Toyota Hiace na Coaster eneo la Kihanga mkoani Kagera.

Ajali hiyo imetokea leo Jumanne, Desemba 3, 2024 katika Barabara ya Kihanga-Kyaka eneo linalotumiwa na maofisa wa idara ya uhamiaji kwa ajili ya ukaguzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na uzembe wa dereva.

“Majira ya saa 5.00 asubuhi imetokea ajali mbaya iliyohusisha lori aina ya Scania likiwa linatokea Kihanga kwenda Kyaka, alipofika kwenye eneo hili kulikuwa na magari mawili ya abiria moja Coaster na Toyota Hiace ambazo zilikuwa zimesimama zikiendelea na ukaguzi uliokuwa ukifanywa na idara ya uhamiaji.

“Kwa bahati mbaya Scania lilivyokuwa linashuka kwa uzembe na kutokuchukua tahadhari dereva alikuja akiwa na mwendo mkali, aliigonga Hiace, pia akaigonga Coaster, ajali hiyo imesababisha vifo saba na majeruhi tisa, wanaume wanne na wanawake watano, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe,”amesema Chatanda.

Taarifa zinasema kuwa, miili hiyo saba imehifadhiwa katika Hospitali Wilaya Karagwe na majeruhi wanaendelea na matibabu.

Related Posts