Dar es Salaam. Kupungua mifugo inayopelekwa sokoni, madai ya kuwapo wanunuzi kutoka nje ya nchi katika minada ya awali na ongezeko la mahitaji ya nyama ni miongoni mwa sababu ya zinazotajwa kupaisha bei ya nyama katika maeneo mbalimbali nchini, Dar es Salaam ikiongoza.
Sababu hizo zimechochea kupanda kwa bei ya ng’ombe katika minada ya awali na ya upili, inayotumiwa na wauzaji wa jumla wa nyama kupata mifugo.
Kupanda bei ya ng’ombe kunatajwa kuwaumiza wanunuzi wengi wa rejareja ambao wanalazimika kuingia mifukoni zaidi ili kupata kilo moja ya nyama kwa Sh11, 000 hadi Sh12,000 kutoka bei ya awaly kati ya Sh8,000 hadi Sh10,000 katika maeneo tofauti ndani ya miezi mitatu nyuma.
Hali ikiwa hivyo Dar es Salaam, bei ya nyama katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Arusha nako imepanda kutoka kati ya Sh8, 000 na Sh9, 000 hadi Sh12,000.
Jijini Mwanza kwa takribani wiki moja sasa, kitoweo hicho kimepanda kutoka Sh8,000 hadi kati ya Sh9,500 na Sh10,000.
Tofauti na maeneo hayo, Dodoma bei ni kati ya Sh6, 000 na Sh10,000 ikiwa haijapanda, sawa na Zanzibar ambako bei imeendelea kuwa Sh14,000 kwa kilo moja.
Huko Mbeya, pia nyama imepanda kutoka Sh8, 000 za awali hadi Sh9, 000 katika kipindi cha wiki mbili sasa.
Mfanyabiashara wa nyama jijini Mbeya, Nassoro Mwaiseta amesema ongezeko hilo limesababishwa na kuadimika kwa ng’ombe.
“Kipindi hiki ng’ombe wanasumbua, kuna wafanyabiashara wakubwa wanafuata kwa wafugaji vijijini kwa sisi tunaosubiri machinjioni kuna wakati tunakosa, tunashindwa kabisa kuchinja,” amesema.
Kama ilivyo Mbeya, ufuatiliaji wa Mwananchi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es umebaini ongezeko la bei limetokana na kupanda kwa kitoweo hicho katika machinjio ya Vingunguti.
“Sisi tunanunua kilo moja kwa Sh9, 800 lazima tuongeze ili tupate faida kidogo kwa sababu kuna kodi za kulipa, usafiri wa kuifikisha nyama hapa na maduka yenyewe siyo ya kwetu,” amesema Lazaro Mmasi mfanyabiashara ya nyama eneo la Tabata.
Kauli kama hiyo imetolewa na Goddy Michael, anayeuza nyama Kiluvya, wilayani Ubungo anayeeleza wauzaji wa jumla wameongeza bei wakisema gharama za ng’ombe minadani zimeongezeka.
“Sasa wale wakishanunua ng’ombe kwa bei kubwa mwisho wa siku wakichinja hata sisi watatuuzia bei ya juu ili wapate faida waendelee na kazi zao kila siku. Ikishakuwa hivyo, nasi tunaangalia namna ya kupata faida, hivyo lazima bei itapanda,” amesema.
Muuzaji wa nyama kwa bei ya jumla, Joel Meshack ambaye hufuata ng’ombe minadani, amesema kuongezeka kwa bei kunasababishwa na kupungua kwa mifugo katika minada ya awali.
Amedai pia kwenye minada hiyo ya awali wameingia wanunuzi kutoka nje ya nchi na kufanya mifugo hiyo ipande bei.
Meshack anasema kabla mvua hazijaanza kunyesha kulikuwa na ukame katika maeneo mbalimbali, hivyo malisho yaliadimika na kusababisha mifugo inayopelekwa mnadani kupungua.
Wakati mifugo ikiwa michache, amesema wanunuzi kutoka nje ya nchi wamekuwa wakiingia katika minada ya awali ambako hawaruhusiwi, bali hutakiwa kuifuata katika minada ya upili iliyowekwa na Serikali.
“Tunapokwenda kwenye minada tunakutana na watu kutoka DR Congo, Comoro wananunua ng’ombe huko kwenye masoko ya awali, yaani kwa wafugaji. Tunapambana nao kwenye manunuzi, wanatubana na kwao masoko yako juu wanachukua bidhaa kwa bei kubwa hii inaongeza ushindani,” amesema Meshack.
Kwa mujibu wa Meshack, ng’ombe mwenye uzito wa kilo 100 na zaidi aliyekuwa akiuzwa Sh1 milioni Machi hadi Aprili, mwaka huu sasa wanamnunua kwa Sh1.2 milioni hadi Sh1.5 milioni hali inayowalazimu kuuza nyama kwa jumla Sh9,700 hadi Sh10,000 kwa kilo moja.
“Tunafanya hivi ili urudishe hela yako kesho uingie kazini, mwisho wa siku wanaoumia katika hili ni walaji wa mwisho,” amesema.
Kukua soko la ndani kutokana na kuongezeka kwa ulaji nyama, pia ni sababu inayotajwa ya kupaa kwa bei ya kitoweo hicho, tofauti na miaka ya nyuma, hasa katika miji mikuu kama vile Dar es Salaam na Dodoma.
Alipokuwa akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mei mwaka huu, Waziri Abdallah Ulega alisema katika mwaka 2023/2024 ulaji wa mazao ya mifugo kwa mtu kwa mwaka uliongezeka, akisema ulaji nyama ulitoka kilo 15 mwaka uliotangulia hadi kilo 16.
Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), John Chasama alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia ongezeko hilo la bei amesema: “Tunalifanyia kazi tutawapa taarifa itakapokuwa tayari.”
Kuhusu wanunuzi kutoka nje ya nchi kuingia kwenye minada ya awali, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael amesema kwa mara ya kwanza walipokea malalamiko hayo mwishoni mwa mwaka jana na waliyafanyia kazi kupitia ofisi zao za kanda na hali hiyo ikakoma.
Hata hivyo, amesema hivi karibuni wamepokea malalamiko hayo tena, kuwa wageni wanaonekana kwenye minada ya Ruvu na wameshaanza kushughulikia suala hilo.
“Lakini hili la wageni linaweza kuonekana kwa namna nyingine, kama ni wageni kutoka nje tunaweza kuona hili katika usafirishaji nje ya nchi,” amesema.
Amesema baada ya kufanya ufuatiliaji ndani ya ofisi yake, hakuna takwimu za ongezeko la mifugo inayosafirishwa kwenda nje kwa mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kilichotangulia.
“Pia hata takwimu zinaonyesha mifugo haijapungua sokoni, idadi imekuwa ileile lakini gharama ndiyo imeongezeka. Hii ikiwa na maana kuwa kipindi cha kiangazi kinachoishia, majani yaliadimika na wafugaji walitumia gharama kubwa kuhudumia mifugo yao, hivyo kufanya bei kuwa juu,” amesema.
Michael amesema hali hiyo inaweza kuanza kupungua baada ya baadhi ya maeneo kupata mvua na huenda inaweza kuwa nzuri kuanzia Januari 2025.
Kwa upande wa mauzo ya nyama nje ya nchi, takwimu za Wizara ya Mifugo zinaonyesha hadi Aprili 2024 tani 13,745.38 ziliuzwa ikilinganishwa na tani 12,243.8 ziliouzwa mwaka 2022/2023.
Kiasi kilichouzwa hadi Aprili mwaka huu kiliingizia nchi Sh149.9 bilioni ikilinganishwa na Sh137.5 bilioni mwaka 2022/2023.
Kati ya kiasi kilichouzwa, nyama ya ng’ombe ilikuwa tani 1,024.33, ya mbuzi tani 9,982.67, kondoo (tani 3,195.09), kuku (tani 32.35) na tani 10.94 za nguruwe.
Msimu kama huu huenda ukawa ni kawaida kwa bei ya nyama kuongezeka lakini si kwa kiasi ambacho kimeonekana sasa.
Takwimu za mauzo za mwenendo wa bei ya wastani ya mifugo katika mnada wa Pugu inayotolewa kila wiki na Bodi ya Nyama Tanzania, inaonyesha katika wiki hii ya kwanza ya Desemba bei zimekuwa zikiongezeka.
Kwa mfano, takwimu za wiki ya kwanza zilizotolewa Desemba 7, 2023, ng’ombe mwenye uzito wa kilo 80 na zaidi alikuwa anauzwa kwa Sh640,000 ambayo ilikuwa ongezeko kutoka Sh597,500 za wiki ya mwisho ya Novemba mwaka jana; wa kilo 200 na zaidi aliuzwa kwa Sh2.6 milioni kutoka Sh2.09 milioni wiki iliyotangulia.
Jambo hilo limeonekana tena katika wiki hii ya kwanza kwa takwimu za Desemba 2, 2024 kuwa ng’ombe wa uzito wa kilo 80 na zaidi aliuzwa Sh800,000 akishuka kutoka Sh900,000 wiki ya mwisho ya Novemba mwaka huu, huku ng’ombe wa kilo 200 na zaidi akifika Sh3.5 milioni kutoka Sh2.5 milioni wiki ya mwisho ya Novemba.
Hii ikiwa na maana kuwa bei ya ng’ombe katika mnada wa upili wa Pugu katika wiki ya kwanza ya Desemba mwaka huu ilioongezeka kwa asilimia 25 kwa yule wa kilo 80 na asilimia 34.6 kwa ng’ombe wa kilo 200 na zaidi ikilinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana.
Katika hili, Michael anasema ongezeko la bei wakati mwingine linaweza kuchochewa na uhitaji wake kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
Hali hiyo pia inaweza kuchangiwa na upungufu wa mifugo inayoingia sokoni katika msimu husika ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo.