Huenda katika mazingira fulani kwa bahati mbaya umewahi kupata changamoto ya kutamka kwa isivyo sahihi baadhi ya maneno, na kujikuta unakosea baadhi ya herufi.
Hali hii ndio tafsiri ya “kuchapia”.Zipo sababu mbalimbali zinazochochea kuibuka kwa kwa hali hii ikiwemo kutokea kwa bahati mbaya yaani isivyo tarajiwa wakati wa kipindi cha mazungumzo.
Lakini zipo sababu zingine ambazo huchagiza kutokea kwa hali hii, mbali na ile hali isiyo tarajiwa yaani bahati mbaya.
Athari ya lugha ya kwanza pia huchangia kutokea kwa hali hii, kwani unakuta mzungumzaji anapotamka maneno ya Kiswahili anachanganya na neno au maeneo ya lugha yake ya asili au ya kikabila. Mathalani, mtu anasema, fiatu fyangu badala ya viatu vyangu.
Vilevile kutamka kwa kasi au kwa haraka pia husababisha ‘kuchapia’ kutokana na kukosekana kwa mpangilio mzuri wa maneno wakati wa utamkaji.
Kwa mfano, mtu anasema Serikali imebwinu mbinu badala ya kusema Serikali imebuni mbinu. Pia mtu anasema Tanzania inachumba chima badala ya Tanzania inachimba chuma.
Kupitia mifano hii inaonesha hali iliyowafanya watamke maneno pasipo usahihi, ni kuzungumza kwa kasi au kwa haraka kunakosababisha kukosekana kwa mpangilio mzuri wa maneno wakati wa uzungumzaji na kujikuta wakitamka maneno isivyofaa.
Kuzungumza au kutamka maneno pasi na usahihi (kuchapia) muda mwingine huwa ni sehemu ya kusisimua au kuburudidha baina ya wazungumzaji.
Mtu anapochapia wale wanaozungumza aghalabu huangua kicheko, kwa kile walichokisia kutokana na mtu kutamka isivyofaa.
Wale wenye moyo mdogo wa kuvumilia kicheko, huweza kukatisha mazungumzo kabisa na kuamua kuondoka eneo husika kutokana na kule kuchekwa baada ya kuchapia.
Tukija upande wa pili wa shilingi, unaonesha kuwa kuendelea kutokea kwa hali hii, muda mwingine huweza kuibua migogoro baina ya wazungumzaji kwani mtu anapochapia mara nyingi wale anazungumza nao huangua kicheko na wengine huamua kuigiza neno au maneno yaliyo tamkwa isivyofaa na mzungumzaji husika.
Sasa muda mwingine mzungumzaji aliyechapia anakuwa hapendwi na kuchekwa kule, hivyo hukasirika na muda mwingine kukatisha kabisa mazungumzo.
“Jicho la Kiswahili” linaona kuwa ili kulinda uhai na ustawi wa lugha ya Kiswahili, tunapaswa kufanya juhudi anuwai katika kukabiliana na hali hii inayojitokeza katika mazungumzo ya Kiswahili.
Mosi, wazungumzaji wanapaswa kutamka maneno kwa mtiririko mzuri unaokubalika kulingana na sarufi ya Kiswahili, kwani kutamka isivyofaa hasa kutamka kwa haraka, ni moja ya sababu inayoibua kuchapia.
Pili, kwa wale wazungumzaji wa Kiswahili ambao kwao Kiswahili ni lugha ya pili, wanapaswa kuwa makini pindi wanapozungumza Kiswahili ili kutochanganya maneno ya lugha za kikabila na Kiswahili.
Hata hivyo, natambua kuwa lugha hizo zote ni miongoni mwa lugha za Kibantu ambazo kuna mfanano kwa baadhi ya vipengele ikiwemo msamiati wa lugha.