Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
PAMOJA na mchango wa Sekta ya Maliasili na Utalii katika uchumi wa nchi na ustawi wa jamii Sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuongezeka kwa migongano baina ya binadamu na wanyamapori inayosababishwa na uvamizi wa shughuli za binadamu karibu na maeneo ya hifadhi na kwenye shoroba za wanyamapori hususan shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ya kudumu.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana ameyazungumza hayo leo wakati wa semina ya maafisa wanyamapori wa Wilaya Nchini iliyofanyika jijini Dodoma ambapo amesema swala hilo linapelekea kuzibwa kwa shoroba za wanyamapori, kuongezeka kwa vitendo vya ujangili wa nyamapori, na migogoro ya mipaka ya hifadhi na vijiji vinavyozunguka maeneo yaliyohifadhiwa.
“Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto za uhifadhi nchini ikiwa ni pamoja na kuandaa Sera, Kanuni, Mikakati, Mipango na Miongozo mbalimbali” – Dkt Chana.
Waziri Chana amesema Wizara inatambua mchango mkubwa wa Maafisa Wanyamapori wa Wilaya katika kutekeleza Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 na Sheria ya Wanyamapori Sura ya 283.
” Itakumbukwa kwamba katika utekelezaji wa Sera na Sheria hizo mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori katika ngazi ya Wilaya yamekasimiwa kwa Maafisa wanyamapori wa Wilaya kwa mujibu wa kifungu Na. 7 (6) cha Sheria ya Wanyamapori, ikiwemo usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMA)”
Aidha Dkt Chana amesema wanatambua kwamba wanyamapori hao wamekuwa wakitekeleza jukumu hilo muhimu la usimamizi wa wanyamapori .
Wizara ya Maliasili na Utalii inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa shughuli za uhifadhi.
“Katika kutekeleza kwa vitendo Falsafa ya 4Rs ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding), na kwa kutambua mchango wa uhifadhi katika ngazi ya Wilaya, na changamoto zake, Wizara imeandaa Semina ya siku mbili kuanzia leo na kesho” – Balozi Chana
Mwisho Waziri Chana amewataka maafisa wanyamapori hao kutumia Semina hiyo kujadiliana mbinu mbalimbali za kuendeleza uhifadhi na kutatua changamoto zinazokabili uhifadhi wa wanyamapori nchini na tutaweka mikakati ya namna bora ya kuendeleza utekelezaji wa majukumu ikiwemo kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika maeneo yao ya kazi.