KIBARUA kijacho Yanga ni pale Algeria kwa ajili ya mechi yake ya pili ya Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger, lakini mashabiki wakiwa hawana amani hasa kutokana na viwango vya nyota wao ikiwemo Stephane Aziz Ki na Prince Dube.
Baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara ikilala 1-0 dhidi ya Azam na 3-1 dhidi ya Tabora United, Yanga ilikumbana na kipigo cha tatu mfululizo katika michuano yote ilipolala kirahisi 2-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Yanga ilishinda ugenini mechi iliyopita ya ligi 2-0 dhidi ya Namungo, lakini morali ya timu na viwango vya nyota wake ndio vinavyowanyima raha mashabiki katika mechi hiyo ijayo kwenye moja ya ardhi zenye mashabiki watata sana Uarabuni, Algeria.
Kati ya mijadala mikubwa katika soka nchini kwa sasa ni kiwango cha mshambuliaji aliyesajiliwa kwa mbwembwe kutoka Azam FC, Prince Dube.
Straika huyu wa Zimbabwe alianza maisha Yanga kwa moto mkali kabisa, sawa na Aziz alivyouanza msimu huu kibabe.
Alifunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya TS Galaxy, timu ya zamani ya kocha wa sasa wa Yanga, Sead Ramovic, shukrani kwa asisti ya Aziz Ki katika za pre-season nchini Afrika Kusini.
Na katika mechi ya fainali ya Kombe la Toyota, ambayo Yanga ililitwaa kwa kuichaka Kaizer Chiefs 4-0 kule Sauzi, Dube alifunga bao la kwanza na kutoa asisti ya bao la tatu kwa Clement Mzize, wakati pia alitengeneza nafasi ya bao la pili lililofungwa na Aziz Ki aliyemalizia asisti ya Duke Abuya. Aziz pia akafunga bao lake la pili na la nne kwa Yanga baada ya kumchekecha beki hadi akakaa chini kabla ya kuuweka mpira wavuni.
Aziz pia alifunga bao moja la penalti na kutoa asisti ya kona kwa Mudathir Yahya katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Red Arrows katika tamasha la Siku ya Mwananchi.
Katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga iliilaza Simba 1-0, Dube aligongesha nguzo ya lango kabla ya kutoa asisti ya bao la ushindi kwa Maxi Nzengeli.
Na katika fainali ya Ngao ya Jamii, Dube alifunga bao la kwanza la Yanga dhidi ya waajiri wake wa zamani Azam FC katika ushindi wa 4-1, huku Aziz Ki akifunga la pili, huku mengine yakifungwa na Clement Mzize na la kujifunga la Yoro Diaby.
Katika mabao yale 17-0 ya mechi nne za kufuzu hatua ya makundi, Dube alifunga matatu na asisti moja, wakati Aziz Ki alifunga mabao manne na asisti moja, huku Clatous Chama katika mechi moja pekee dhidi ya Vital’O alitoa asisti nne na kufunga bao moja la frii-kiki iliyokwenda moja kwa moja wavuni wakati Yanga ikishinda 6-0.
Clement Mzize, Mudathir Yahya, Kennedy Musonda, Duke Abuya, Pacome Zouzua, Maxi Nzengeli, Chama, Dube, hawa wote na wengine walifunga katika mechi hizo ambazo Yanga ilikuwa katika ubora wake.
Timu hiyo ya wananchi ilitishia wapinzani kwa sababu mabao yalikuwa yakitokea kila upande hadi kwa mabeki akiwamo Ibrahim Bacca aliyefunga mfululizo kwenye ligi.
Ndio maana leo kusema Aziz KI na Dube tu ndio chanzo cha kukwama kwa Yanga, sio sahihi. Ni tatizo la kushuka kiwango kila takribani kila mmoja. Kwa kikosi cha sasa, ni ngumu kusema ni mchezaji gani yuko katika ubora wake aliokuwa nao wakati wa kuanza kwa msimu.
Majeraha kwa baadhi ya nyota na uchovu wa mechi nyingi mfululizo vinaweza kuwa kati ya sababu za kushuka kwa viwango vya wachezaji wengi huku, lakini lipo jambo jingine muhimu ambalo sio la kupuuzwa – kushtukiwa kwa mbinu ya kumiliki sana mpira.
Mamelodi Sundowns walishikiliwa kwa sare ya bila mabao dhidi ya timu inayoshiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Union Maniema ya DR Congo kwenye Uwanja wa nyumbani wa Loftus Versfeld mjini Pretoria.
Miamba ya Afrika Kusini, Mamelodi ni timu inayojulikana na kumiliki mpira kwa asilimia kubwa na ni kosa kubwa kushindana nao kumiliki mpira kwani hiyo itakula kwako.
Ndio maana timu zinazojielewa hazithibutu kufuata njia zao za mchezo, zinajaza wachezaji katika kujilinda na kupata matokeo. Yanga pia ilicheza hivyo mechi zote mbili dhidi ya Mamelodi katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita na nusura ipate matokeo kama sio bao la Stephane Aziz KI kukataliwa kiutata kule Pretoria
Hii ndio sababu kubwa katika mechi yao ya kwanza ya Kundi B Novemba 26, 2024, Mamelodi iling’ang’aniwa kwa suluhu na timu ambayo wengi waliamini ingeshushiwa mvua ya mabao ya Maniema.
Katika mechi hiyo, Mamelodi ilimiliki mpira kwa asilimia 77 dhidi ya 23 za Maniema, ikapiga mashuti 17 lakini yaliyolenga lango yalikuwa matano tu, dhidi ya mashuti manane ya Maniema huku kukiwa na hamna lililolenga lango.
Hizi ni aina ya takwimu zinazoshabihiana na za Yanga dhidi dhidi ya Al Hilal. Siku ile Jumanne ya Novemba 26, 2024 kwa Mkapa, Yanga ilitawala mchezo kwa asilimia 63 dhidi ya 37 za Al Hilal, huku timu ya wananchi ikipiga mashuti 14 lakini ni manne tu yaliyolenga lango, dhidi ya mashuti sita ya Al Hilal.
Kati ya mashuti sita ya Al Hilal, ni mawili tu ambayo yalilenga lango na yote yaliingia wavuni na kuizamisha Yanga kwa mabao 2-0.
Kocha Florent Ibenge ni mzoefu. Alijua Yanga ni timu ambayo imetisha katika miaka mitatu iliyopita ikishinda takriban mataji yote ya ndani na ikaingia msimu huu ikiwa imesajili mafundi wa kuifanya itishe zaidi.
Kwa uzoefu alionao alitambua kwamba timu ambayo imeingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa ushindi wa mabao 17-0 katika mechi nne za hatua ya mchujo, sio timu ya kuichukulia poa na kushindana nayo kupiga pasi. Akaiachia mpira, yeye akabaki na ushindi.
Kocha Sead Ramovic siyo mzoefu wa levo hii ya mashindano kwa sababu hajawahi kuiongoza timu ya kiwango kama cha Yanga na tena kwenye michuano kama hii.
Hili ni moja ya mambo ambayo anaweza kujisahau nayo akajikuta anapata wakati mgumu katika mechi nyingi sana, kwa sababu unapokuwa mazoezini na wachezaji wa kiwango cha juu, unaweza kuona kwamba una uwezo wa kufungua kila mlango wa upinzani na kupata mabao mengi.
Lakini haiko hivyo kwa sababu wapinzani wengi kwa soka la sasa huifutilia timu kabla ya kukutana nayo. Na kama wameisoma Yanga katika siku za hivi karibuni, wanajua kwamba kushindana nayo kumiliki mpira ni ni kuwapa nafasi mastaa wake kuonyesha ubora wao. Hili si jambo ambalo makocha wengi huruhusu, wengi hutaka kuhakikisha kila mchezaji mzuri wa upinzani hapati nafasi ya kuonyesha vitu vyake, hivyo hufunga duka kwa kuwaachia mcheze mtakavyo kwenye maeneo ambayo sio hatarishi lakini wakiziba njia zote muhimu za kuwadhuru.
Kama Ramovic hatashitukia hilo na kutumia mbinu mbadala ikiwamo kutanua uwanja kwa kuwatumia mawinga na pia kupunguza kumiliki mpira ili kuwatamanisha wapinzani kuvutika mbele kuja kusaka mabao na hivyo kuacha mianya ya kukimbia nyuma yao, basi atakuwa na wakati mgumu sana katika mechi hii ya Jumamosi dhidi ya MC Alger na nyinginezo kama ilivyokuwa dhidi ya Al Hilal. Nini maoni yako.