Unguja. Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar imesema Serikali inatambua changamoto tofauti ya ukokotoaji wa mafao ya kiinua mgongo hasa kwa wafanyakazi walioajiriwa kuanzia mwaka 1989/98.
Kutokana na hilo, imeunda timu ya wataalamu kuangalia changamoto hiyo kama ilivyobainishwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juma Makungu Juma leo Jumanne Desemba 3, 2024 katika mkutano wa 17 wa Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman.
Dk Mohammed ametaka kujua ni kwa kiasi gani Serikali inatambua malalamiko ya changamoto ya wastaafu kuhusu ukokotoaji wa mafao ya kiinua mgongo na pensheni kutokana na mfumo unaotumiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar(ZSSF).
Makungu amesema Serikali imeunda timu ya wataalamu wa kuiangalia changamoto hiyo na baadaye itafanya uamuzi ili kuweka uwiano katika mfumo wa ukokotoaji na kuondoa malalamiko yaliyopo.
“Katika kuitatua changamoto hiyo, Serikali imeunda timu maalumu ya kuishughulikia changamoto hiyo na kuitafutia njia bora ya kuitatua,” amesema Makungu.
Amesema katika ukokotoaji wa mafao kwa wastaafu, ZSSF inatumia mifumo miwili, kati ya mifumo hiyo moja ni ukokotoaji wa mafao kwa kuangalia mchango wa mwanachama aliochangia na ukokotoaji wa mafao kwa mujibu wa fomula ambao mfumo huu unaangalia muda wa mwanachama aliochangia, mshahara unaotumika na uwiano wa kima cha mafao.
Hata hivyo, amesema kwa Zanzibar wanatumia mfumo wa ukokotoaji wa mafao kwa njia ya fomula kwani ndio ulioanishwa katika sheria, pia wanazingatia mfumo wastani wa mshahara kwa mstaafu ya miezi sita ya mwanzo katika miezi 156.
Pia, amesema wanazingatia uchangiaji wa mwanachama, muda wa uchangiaji pamoja na uwiano wa kima cha mafao kwa asilimia 36 kwa miaka 13 ya mwanzo na kila mwaka ukiongezeka na kiwango kinaongezeka kwa asilimia mbili.
Akitoa hotuba yake Mei mosi, mwaka huu, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi alisema Serikali kupitia ZSSF imetekeleza ahadi ya mwaka 2022 ya kutoa mafao mawili mapya kwa ajili ya wanachama wake miongoni mwa mafao hayo ni fao la kuumia kazini na fao la upotevu wa ajira.
“Napenda niwaarifu wafanyakazi kwamba ahadi hiyo imeanza kutekelezwa na sasa ZSSF wameanza kutoa mafao hayo,” amesema Dk Mwinyi.
Pia, ameahidi kupandisha kima cha chini cha pensheni kwa wastaafu wanaopokea pensheni chini ya Sh180, 000 na hilo limefanikiwa kutekelezwa na mfuko huo umeanza kuwalipa wastaafu wote kima cha chini cha pensheni kuanzia Sh180,000.
Amesema kwa kuzingatia wafanyakazi wanaostaafu kwa hiari wakiwa na umri wa miaka 55 wanapata kiinua mgongo pungufu tofauti na wale wanaopokea wakistaafu kwa lazima wakiwa na umri wa miaka 60.
Hivyo, Serikali imeshaiagiza ZSSF kufanya tathmini juu ya hilo ili wafanyakazi wanaostaafu kwa hiari wakiwa na miaka 55 wapate kiinua mgongo bila upungufu.