TARIQ: Nimefungulia njia ya mabao

LICHA ya Kagera Sugar kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mashujaa katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma kilichompa faraja mshambuliaji Tariq Seif  ni kufunga bao lake la kwanza na baada ya hapo kasema ni kama amefungua njia ya mafanikio mengine.

Kagera ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Tariq katika dakika ya 30 kabla ya Mashujaa kusawazisha dakika ya 87 kwa mkwaju wa penalti  kupitia kwa Mohamed Mussa, nyota wa zamani wa Malindi ya Zanzibar na Simba.

Tariq alisema ilikuwa inamuumiza kuona mzunguko wa kwanza ungemalizika bila kucheka na nyavu kwani licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara, lakini dakika chache anazopata anatamani kufanya vitu vya kukumbukwa.

“Kazi ya mshambuliaji ni kufunga mabao inaumiza sana kuona mabeki wanafunga halafu sijafunga. Naamini nimepata mwanzo mzuri kilichobaki ni kuendelea kupambana. Bado safari inaendelea,” alisema.

Msimu uliopita Tariq alimaliza na mabao matano na alilofunga dhidi ya Azam FC katika mechi ya Februari 16, 2024 timu hiyo ikifungwa mabao 2-1 liliingia kuwania tuzo ya bao bora la msimu.

Related Posts