Songea. Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) limetoa huduma za upimaji wa Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa watu 89,602 waliopo gerezani huku 2,030 wakigundulika na maambukizi katika kipindi cha Oktoba 2023 hadi Septemba 2024.
Upimaji huo uliofanyika kupitia mradi wa USAID Police and Prisons Healthcare ulifanikisha kugundua watu 1,362 kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu na kupatiwa matibabu stahiki.
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani katika viwanja vya Majimaji mjini Songea, Mkurugenzi wa Miradi wa THPS, Dk Eva Matiko amesema THPS ilifanikisha hilo kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wakishirikiana na Serikali.
“Kupitia mradi huo, watu 2,697 walianzishiwa na kukamilisha dawa kinga dhidi ya kifua kikuu, wakiwamo watu wanaoishi na VVU na watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao walikuwa wanaishi na watu wenye ugonjwa wa kifua kikuu,” amesema Dk Matiko.
Amesema katika kipindi hicho, THPS kupitia mradi wa PEPFAR/CDC Afya Hatua, ilitoa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa jumla ya watu 1,170,902 na 17,989 walibainika kuwa na virusi.
Aidha, amesema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024, watu 190,311 walipata huduma ya dawa za kufubaza makali ya VVU kupitia vituo vya afya 350 vilivyofadhiliwa na mradi huu.
“Vilevile, watu 1,731 walikamilisha matibabu ya kinga dhidi ya kifua kikuu, na wanawake 67,914 wanaoishi na VVU walipokea huduma ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi katika mikoa ya Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga,” amesema.
Amesema THPS imepanga kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
“Mradi huu ulitoa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa waathirika 52,978, na 47,633 walikuwa waathirika wa unyanyasaji wa kimwili au kihisia na 5,345 walikuwa wa unyanyasaji wa kijinsia,” amesema Dk Matiko.
Pia, amesema walitoa huduma za tohara kinga kwa wanaume 165,711 katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga.
“Wasichana rika balehe na wanawake vijana 33,313 walinufaika na mpango wa DREAMS katika Mkoa wa Shinyanga, unaolenga kutoa huduma za afya na kuzuia maambukizi kwa wasichana na wanawake vijana,” amesema Dk Matiko.
Katika hatua nyingine Patricia Kuya, Ofisa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi anayesimamia huduma za vijana Wizara ya Afya kutoka NASHCoP kupitia mpango wa kudhibiti Ukimwi, amewataka wazazi kuanza kuzungumza na watoto wao kwa uwazi na kuacha kuogopa kwa kisingizio cha mila na desturi.
Kuya amesema kwa vijana wa umri wa miaka tisa hadi 24 takwimu zinaonyesha ndio kundi kubwa linaloongoza kwa kuwa na maambukizi mapya ya VVU.
Amesema, elimu iliyotolewa kwa wazazi, vijana, watoa huduma ngazi ya jamii, viongozi wa jamii na walimu imesaidia kuwaelimisha wazazi juu ya mapambano dhidi ya Ukimwi na kuepusha wasijiingize kwenye vitendo vya ngono zembe ili kuwalinda wasiambukizwe virusi.
Amesema tayari wazazi na vijana 350,000 kutoka halmashauri 18 za mikoa mitano nchini zimefikiwa na afua hiyo imepokewa vizuri, itakayosaidia wazazi kuwaelimisha watoto na vijana namna ya kujikinga na maumbukizi ya magonjwa ya ngono, homa ya ini na tabia hatarishi zinazoendelea katika jamii kama utumiaji wa dawa ya kulevya sigara na pombe.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na VVU (Nacopha) Leticia Mourice ameitaka jamii kubadili tabia, kupiga vita unyanyapaa, kutambua na kuwatetea wote wanaonyanyaswa kijinsia, kutambua na kupiga vita kila aina ya vikwazo vya kijamii vinavyohatarisha makundi mbalimbali.
Amesema, jitihada za Nacopha zinaendelea kuimarika kwa kuhakikisha makundi yote yenye mahitaji maalumu yanafikiwa.