Trafiki walivyojipanga kudhibiti ajali mwishoni mwa mwaka

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani (Trafiki) limetaja mikakati mitano ya kudhibiti ajali hasa za mwisho mwa mwaka.

Mkuu wa Trafiki nchini, Kamanda Ramadhani Ng’anzi ametaja mikakati hiyo ikiwamo kuongeza kamera ‘tochi’ ili kudhibiti ajali za barabarani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 3, 2024 jijini Dar es Salaam, amesema askari wenye kamera watakaa maeneo mbalimbali, yakiwamo ya kificho.

Amewataka Watanzania kutowapangia sehemu za kukaa wakati wa kutekeleza jukumu hilo la kubaini mwendokasi wa magari.

Kamanda Ng’anzi amesema mikakati mingine ni kuhakikisha mabasi yanafuata ratiba, kukagua vyombo vyote vya moto, kuongeza askari, kuhakikisha mabasi yanakuwa na madereva wawili na kuangalia mfumo wa kuratibu mwenendo wa mabasi (VTS).

“Hatutajali askari wetu amejificha au kuonekana, tukiona mbinu ya kujificha inatupa matunda tutaitumia au zote mbili hatutaki mtu atupangie tutumie mbinu gani. Lengo letu ni kudhibiti ajali za barabarani,” amesema.

Amesema chanzo kikubwa cha ajali ni mwendokasi na uzembe wa madereva barabarani, hivyo wataimarisha mifumo ya udhibiti wa mwendo, akisema polisi wamejipanga ipasavyo.

Amesema wataongeza idadi kubwa ya askari barabarani, akieleza baadhi ya madereva wakiona polisi wengi wanaogopa, jambo litakalowezesha kuimarisha usalama barabarani.

Kamanda Ng’anzi amesema watakagua mifumo mingi ya magari ikiwamo ya breki na wasiporidhika na gari au chombo cha moto watakizuia kuingia barabarani.

Amewaelekeza makamanda wa kikosi hicho kukamata magari yote mabovu yakiwemo malori yanayotembea na taa moja usiku au magari yenye matairi vipara (yaliyoisha).

“Kutakuwa na vitabu maalumu vya madereva kwenye vituo vitakavyowekwa ili kuhakikisha wanabadilisha usukani, badala mmoja kuendesha umbali mrefu. Tunafanya hivi ili kuwaondolea uchovu madereva wanaotembea zaidi ya saa nane.

“Wale madereva wanaokwenda Kanda ya Ziwa, watabadilisha Singida, wanaokwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini watabadilishana Iringa. Dereva atashuka na kusaini kitabu kisha dereva mwingine atapanda,” amesema.

Kamanda Ng’anzi amesema kumekuwa na utaratibu wa watu kusafiri na familia zao, baadhi wanaendesha magari mapya kwenda nayo mikoani kwa ajili ya mapumziko.

“Nitoe wito wale madereva wasiokuwa na uwezo wa kuendesha umbali mrefu zaidi ya saa nane, ni bora wachukue madereva wazoefu watakaosafirisha familia zao au wahakikishe wanakuwa na muda mzuri wa kumpumzika.

“Ni hatari sana umebeba abiria halafu unatembea kilomita 1,000 uko peke yako, ukifika mahali unasimamia unaagiza chakula, nyama kisha unashushia kinywaji kitakachokufanya mwili wako usiwe timamu,” amesema.

Amesema ili kudhibiti hilo, watatawanya vipima ulevi ambavyo vitatumika kwa madereva wote watakaokuwa barabarani, wakiwamo wa bodaboda.

“Ukibainika kukutwa na kilevi utakaa mahabusu ambazo zimetengezwa kiasi kwamba zinaweza kuondoa kilevi cha aina yoyote,” amesema.

Kamanda Nga’nzi amesema madereva 259, wakiwamo wa magari ya Serikali na kampuni binafsi wamefungiwa leseni kuanzia Januari hadi Novemba 2024 kutokana na kufanya makosa hatarishi barabarani.

Related Posts