UN yatoa wito wa kupunguza uhasama na kuwalinda raia Syria – DW – 03.12.2024

Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa imesema mashambulizi yaliofanywa na muungano wa waasi unaoongozwa na kundi lenye itikadi kali la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) na ambao wameuteka mji wa pili wa Syria wa Aleppo, yanazidisha mateso kwa mamilioni ya watu nchini humo baada ya miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Jeremy Laurence, msemaji wa Kamishna Mkuu wa ofisi hiyo amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa Volker Turk ana wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa  uhasama nchini Syria  tangu Novemba 27, na kwamba hali hii ni ya kusikitisha, kwani raia wengi wa Syria wamekuwa wakiishi kwa taabu tangu vilipozuka vita vya mwaka 2011 wakati rais Bashar al-Assad alipoyazima kwa nguvu maandamano ya kuunga mkono demokrasia.

Waasi wakivurumisha roketi huko Aleppo, Syria
Waasi wakivurumisha roketi huko Aleppo, SyriaPicha: Juma Mohammad/AP Photo/picture alliance

Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imeorodhesha matukio kadhaa yaliyohusisha vifo vingi vya raia, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya wanawake na watoto, vitendo hivyo vikiwa vimeendeshwa na waasi hao au hata vikosi vinavyoiunga mkono serikali. Aidha Jeremy Laurence, msemaji huyo wa Kamishna mkuu wa haki za binaadamu amezitolea wito pande zote kupunguza uhasama.

” Tunaziomba pande zote kupunguza kasi ya mzozo, kuwalinda raia na kuruhusu misaada muhimu kuwafikia  wale wanye uhitaji. Pia, tunatoa wito kwa nchi za kigeni zenye ushawishi kufanya kila waliwezalo ili kuhakikisha  sheria za kimataifa za kibinadamu zinaheshimiwa, kuendeleza mazungumzo na kuzuia kuendelea kwa ghasia hizi ili zisizidishe mateso kwa watu wa Syria na kuchochea mivutano ya kikanda,” alisema Bwana Laurence.

Mapambano yaendelea huko Syria

Uharibifu kutokana na mashambulizi katika mji wa Syria wa Idlib
Uharibifu kutokana na mashambulizi katika mji wa Syria wa IdlibPicha: Bilal Alhammoud/Middle East Images/AFP via Getty Images

Jeshi la Syria na mshirika wake Urusi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya anga katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi hao, na mpaka sasa mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 457, wakiwemo raia zaidi ya 70, takwimu hizi ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la kuchunguza vitendo vya haki za binadamu nchini Syria. Jana Jumatatu, Umoja wa Mataifa ulisema takriban watu 50,000 wameyakimbia makazi yao katika siku za hivi karibuni.

Soma pia: Uturuki: Kiini cha vurugu za Syria si “uingiliaji wa kigeni”

Waasi hao wamesonga mbele hii leo katika mji wa nne kwa ukubwa nchini Syria wa Hama baada ya kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa ya kaskazini mwa Syria.

Mapigano haya ya ghafla ambayo yamemaliza miaka minne ya utulivu nchini Syria, yamepamba moto wakati eneo la Mashariki ya Kati likiwa kwenye mashaka ya kuzuka kwa vita vipana zaidi vya kikanda kutokana na vita vinavyoendelea Gaza na hofu ya kuvunjika kwa makubaliano ya usitishaji mapigano katika nchi jirani ya Lebanon.

(Vyanzo: AP, Reuters, AFP)

Related Posts