Imeelezwa kuwa vikao vya mara kwa mara kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Mkoa wa Lindi vimesaidia kuongeza ushirikiano na kupunguza changamoto kubwa katika ukusanyaji wa kodi Mkoani humo.
Kauli hiyo imetolewa leo Disemba 3,2024 na Matilda Kunega ambaye ni Meneja wa TRA Mkoa wa Lindi wakati hafla fupi ya kukabidhiwa cheti maalum kutoka kwa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania.
Cheti hicho alichokabidhiwa meneja huyo kimetoka kwa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania chini ya usimamizi wa Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwa ni kwaajili ya kutambuzi wa kazi yake bora na ushirikiano alioutoa wakati wa ziara ya kikazi ya Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania ilipotia kusikiliza kero za wafanyabishara katika Mikoa mbalimbali nchini ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu na kuepuka changamoto ikiwamo migomo ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara.
Kunega ametumia nafasi hiyo kuwasihi wadau kujitokeza na kuwa wazi kwa Mamlaka hiyo ili kila mmoja ashiriki katika kuchangia maendeleo yanayoonekana Mkoani Lindi ikiwemo barabara zenye taa nzuri, hospitali, huduma za maji na kadhalika.
‘’Tumekuwa tukiwakumbusha wafanyabisha umuhimu wa kodi na kwanini tunakusanya kodi ikiwemo ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kama shule,barabara na hospitali,tunawatembelea kuwafikia katika maeneo yao kuwapatia elimu ya mlipa kodi na kwakweli wanaelewa wajibu huo,sisi Lindi sio kisiwa lazima tuchangie kwa kiwango kile alichopangiwa’’Alisema Matilda.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoroa Mwanziva ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Lindi kupitia jumuiya yao kuendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo ya ukusanyaji mapato kwani wafanyabiashara ni sehemu ya mchakato wa maendeleo ya Taifa na kwamba wasipokuwa timu moja katika ulipaji kodi nchi haiwezi kusogea mbele kiuchumi.
Kuhusu cheti hicho cha utambuzi wa kazi yake bora Kitaifa amewaomba kuendelea kumuunga mkono ili heshima aliyoipata ambayo inaibeba taswira njema ya Mkoa wa Lindi iendelee kulindwa.
Awali,Mwenyekiti wa Jumuita ya wafanyabiashara Mkoa wa Lindi Ndg. Ahmad Mikapa amesema viongozi wa wafanyabiashara wa Lindi wamepokea cheti hicho wakati wa mkutano mkuu wa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania ambapo jumuiya hiyo imeamua kutoa shukurani kwa baadhi ya viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao wamekuwa wakiwahudumia vizuri wafanyabiashara na waliwapokea vizuri wakati wa ziara katika maeneo yao pamoja na mameneja wa Mikoa ambapo kwa nchi nzima mameneja wawili Njombe na Lindi ndio waliopatiwa .
Naye,Katibu Bi.Angel Kessy,Mwenyekiti wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi na Katibu wa Jumuiya ya wafanyabishara Mkoa wa Lindi amekiri kwa sasa changamoto mbalimbali zinazoibuka zimekuwa zikitatuliwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya Mamlaka ya Mapato na wafanyabiashara jambo ambalo limechangia maendeleo ndani ya Mkoa kwa kiasi kikubwa huku akiomba kuendelea kupewa elimu na kutiwa moyo wafanyabiashara ili waweze kutimiza wajibu huo wa ulipaji wa kodi.