WANAWAKE NYAMAGANA WAPATA MAJIKO YA NISHATI SAFI ETHANOL KUPITIA KAMPENI YA SIKU 16 DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA KUTOKA MOTO SAFI

 

Baadhi ya wanufaika katika picha ya pamoja na mgeni rasmi

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akiongea katika hafla hiyo

Makamu Mkuu wa wa chuo cha SAUT Prof. Costa Ricky Mahalu akiongea katika hafla hiyo

Wanufaika wakifuatilia matukio katika hafla hiyo

Wanufaika wakifuatilia matukio katika hafla hiyo

 

***

Ukiwa ni mwendelezo wa kushiriki kampeni ya siku 16 dhidi ya vitendo vya kupinga ukatili wa kijinsia inayoendelea mama lishe wa kata mbalimbali za wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wamepatiwa majiko 100 ya nishati safi ya ethanol kutoka MOTO SAFI na Barrick na kwa ajili ya kuwapunguzia adha ya matumizi ya nishati isiyo rafiki kwa mazingira ya mkaa na kuni.

 

Katika maadhimisho hayo yanayoendelea Barrick na washirika wake wanaendesha shughuli mbalimbali za kutoa elimu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kutoa mafunzo ya matumizi na nishati safi za kupikia na kugawa majiko ya gesi.

 

Baadhi ya washirika wa Barrick katika maadhimisho ya mwaka huu ni Jeshi la Polisi kupitia madawati ya kijinsia, Halmashauri za wilaya,mashirika yasiyo ya kiserikali ya VSO, LCF, Jadra, Hope for the Girls and Women (HGWT) , kampuni ya wanasheria ya Bowmans na Taifa Gas.

 

Akiongea katika hafla ya kukabidhi majiko hayo iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) jijini Mwanza Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi, ambaye alikuwa mgeni rasmi ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wanawake kufanya shughuli mbalimbali za mikono ili kujiingia kipato kwa kuwa mtu akiwa na kipato anaondokana na utegemezi unaopelekea kunyanyasika kwenye jamii.

 

Amewashukuru wadau wanaoshirikiana na Barrick katika maadhimisho ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia mwaka huu kwa kutoa majiko ya nishati safi ya ethanol ili kutunza mazingira na kuwafanya mama lishe kufanya shughuli zao kwa urahisi na kufanikisha ajenda ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupiga vita mabadiliko ya tabia nchi na uchafuzi wa mazingira.

 

Awali akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Makamu Mkuu wa wa chuo cha SAUT, Prof. Costa Ricky Mahalu, amesema changamoto ya unyanyasaji wa kijinsia ni kubwa katika jamii yetu ambapo tatizo hilo linaathiri ustawi wa wanawake katika nyanja mbalimbli za maisha yao.

“Unyanyasaji huu una athari si tu kwa waathirika pia kwa jamii kwani inakwamisha wanawake kutimiza malengo yao na inakuwa ni kikwazo cha maendeleo endelevu” ,amesema Prof. Mahalu.

 

Mmoja wa wanufaika wa msaada huo Happiness Kalebe ambaye ni mama lishe wa soko la Mkolani akiongea kwa niaba ya wenzake amesema jiko hilo linakwenda kuwaongezea tija katika upishi wake wa chakula na kuhudumia wateja wake.

“Kwa kutumia jiko hili litatufanya tusinunue kuni kwa ajili ya kupikia ambapo nitajiongezea kipato, kipindi cha mvua kama hiki kuna wakati tunanunua kuni zikiwa zimenyeshewa wakati wa kusafirishwa na kutusumbua wakati wa kupika, nawashukuru MOTO SAFI na Barrick kwa kututhamini sisi wanawake”, amesema Kalebe.

 

Mbali na kutoa majiko ya gesi na kutoa mafunzo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kampeni ya washirika hawa inaendelea kwa kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutoa ushauri wa kisheria katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Related Posts