Likizo zinakaribia kuanza, na wazazi wengi wanajiandaa kutoa nafasi kwa watoto wao kuweza kupumzika, lakini pia kuwawezesha kutumia muda huo kwa manufaa.
Kwa wengi, likizo ni muda wa kuungana na familia, lakini pia ni changamoto ya kuhakikisha watoto wanakua na kujifunza, wakiepuka kutumia muda mwingi mbele ya runinga au simu.
Godfrey Shija, mzazi wa watoto watatu mjini Shinyanga, anasema kuwa likizo ni fursa ya kipekee ya kuwa na muda na watoto wake baada ya miezi mingi ya masomo.
“Likizo ni wakati mzuri wa kuungana na watoto, lakini pia ni muda mzuri wa kuendelea na masomo, hata kama hatuko shuleni,” anasema.
Godfrey amemwandalia binti yake Kareni Shija, ambaye anayejiandaa kufanya mtihani wa kitaifa, mwaka 2025, ratiba inayozingatia muda wa kusoma na muda wa kujiburudisha.
“Likizo siyo wakati wa kupumzika pekee, ni wakati wa kujiandaa kwa maisha yajayo,” anasisitiza.
Kareni atapata nafasi ya kupumzika, lakini pia ratiba inahakikisha anajiandaa kwa mitihani. Godfrey pia amepanga familia yake kutembelea Jiji la Mwanza, ambapo watoto watapata fursa ya kujifunza kuhusu utamaduni na maisha ya eneo hilo na kupevuka kimaarifa.
Alfred Kato, mzazi mwingine kutoka Bukoba, ana mtazamo tofauti, japo pia ana lengo moja kuu la kumsaidia mtoto wake, Erick Bujune kugundua na kuendeleza vipaji vyake.
“Erick anapenda sana sanaa, na likizo ni wakati mzuri wa kumsaidia kukuza kipaji chake,” anasema.
Alfred amemuandaa Erick kujiunga na kozi ya sanaa ili kuimarisha ujuzi wake wa uchoraji. “Ningependa kuona Erick akitumia likizo hii vizuri, kujifunza zaidi na kuchora picha za ubunifu,” anasema.
Kwa upande mwingine, Muzamiru Katunzi, mwanafunzi kutoka Shinyanga, anaendelea na mazoezi ya soka chini ya uangalizi wa mama yake, Stella Hamurungi.
Stella anaamini kuwa mazoezi ya michezo ni muhimu kwa ukuaji wa kimwili na kiakili wa watoto.
“Muzamiru anapenda soka, na likizo hii ni fursa nzuri ya kumsaidia kukuza ujuzi wake,” anasema Stella. Aidha, Stella amewapa watoto wake majukumu ya nyumbani ili kuwafundisha umuhimu wa kuwajibika.
Wazazi hawa wamesema kuwa ni muhimu watoto wanapokuwa likizo, wawe na shughuli zinazowafanya kuwa na maadili mazuri na kuendelea kujifunza.
Anderson Mkindi, mtaalamu wa mipango ya likizo kutoka Nairobi, anasema kuwa mapumziko baada ya masomo ni fursa ya kipekee ya watoto kugundua vipaji vyao na kujifunza mambo mapya.
“Ni vizuri watoto wafanye shughuli za kimaendeleo kama vile sanaa, michezo, au hata masomo ya ziada,” anasema Mkindi.
Anaongeza kuwa likizo siyo tu ya kupumzika, bali pia ni wakati mzuri wa kuwasaidia watoto kuendelea kujifunza na kugundua mambo mapya.
Hawa niliozungumza nao ni wazazi wa Shinyanga na Bukoba, naamini huo ndio mtazamo wa wazazi wengi katika maeneo mengine.
Aidha, wazazi hawa wanasisitiza kuwa, hata wakati wa likizo, usalama wa watoto lazima uwe kipaumbele.
Esther Makoye, mzazi kutoka Shinyanga, anasema kuwa ni muhimu kwa wazazi kuweka mazingira ya salama kwa watoto wao, hasa wanapokuwa wanacheza au kutembelea maeneo ya umma.
“Kuna hatari za watoto kutokuwa salama katika maeneo ya wazi, na ni jukumu letu kuhakikisha wanakuwa salama,” anasema Esther.
Anaongeza kuwa ni muhimu kwa watoto kuelewa jinsi ya kusema “hapana” wanapohisi wanahatarishwa hasa kipindi hiki ambapo wanaume wasio na maadili, hutumia muda huo kuwarubuni watoto wa kike na mwishowe hurudi shuleni wakiwa na ujauzito, suala ambalo anasema limekithiri mkoani Shinyanga.
Esther pia anasisitiza kuwa wazazi wanahitaji kuwa makini na hali ya mtoto wao wakati wa likizo, kwani wakati mwingine watoto wanaweza kuficha siri kwa wanayofanyiwa na watu wa familia, marafiki au majirani.
“Watoto wanahitaji kujua kuwa, ikiwa mtu yeyote atawataka wafanye jambo lisilo salama, wanapaswa kusema ‘hapana’ na kuwaambia wazazi wao mara moja,” anasema.
Stella Hamurungi na Godfrey Shija wanasisitiza umuhimu wa kuwa na mawasiliano ya wazi na watoto wao wakati wa likizo.
“Ni muhimu watoto wanapokuwa likizo, wajue kuwa wanapokuwa na maswali au wasiwasi, wanaweza kuzungumza na sisi bila woga,” anasema Stella.
Hii inawasaidia watoto kuwa na uwezo wa kutatua changamoto zao na kujikinga na hatari zinazoweza kujitokeza.
Wakati watoto wanapokuwa likizo, ni fursa nzuri kwa wazazi kujumuika nao katika shughuli za kijamii na familia.
Hii inawasaidia watoto kuwa na uhusiano mzuri na wazazi wao na kuwa na hali nzuri ya kiakili. Wazazi katika manispaa za Shinyanga na Bukoba wanatambua kuwa likizo siyo tu ya kupumzika, bali ni wakati muhimu wa kujenga uhusiano imara na familia pamoja na jamii.
Niseme tu kwamba likizo za shule ni fursa kubwa kwa watoto kujijengea misingi imara ya mafanikio ya kitaaluma wanaporudi shuleni.
Hii ni nafasi nzuri ya kujitahidi zaidi katika masomo, na wazazi wanapaswa kuhakikisha kuwa watoto wao wanajifunza mambo mapya wakati wa likizo.
Watoto wanaweza kutumia wakati huu kutembelea maktaba za karibu ili kusoma vitabu na kuongeza maarifa yao. Hii itawasaidia kurudi shuleni wakiwa na uelewa zaidi na kujiamini katika masomo yao.
Kwa mfano, kufanya mazoezi ya kusoma, mazoezi ya kubungua bongo na kufumbua mafumbo, kutawasaidia kuwa na akili za haraka na za ubunifu.
Wanasaikolojia wanasisitiza kuwa watoto wanapojitahidi kupanua msamiati wao na kuongeza ufanisi wa kuelewa, wanakuwa na uwezo bora wa kujifunza kwa urahisi.
Dk. Maria Montessori, mtaalamu maarufu wa elimu, anasema: “Watoto wana uwezo wa kujifunza na kufikia viwango vya juu wakiwa na mazingira bora na yenye changamoto.”
Hivyo, shughuli za kuboresha msamiati wao na kufanya mazoezi ya kukumbuka maneno mapya ni muhimu kwa maendeleo yao.
Mtaalamu mwingine, Profesa Jean Piaget, aliyejulikana kwa utafiti wake kuhusu maendeleo ya akili za watoto, anasisitiza umuhimu wa kutoa changamoto kwa watoto ili wafaulu katika kujifunza. “Mtoto anapojifunza kupitia shughuli za kimantiki na za ubunifu, anajenga misingi ya ufanisi katika masomo,” alisema.
Hivyo basi, likizo sio tu ni muda wa kupumzika, bali pia ni wakati wa watoto kujifua kielimu. Kwa kuendelea kuboresha msamiati wao, kusoma vitabu, na kufanya mazoezi ya kimantiki, watoto wataweza kurudi shuleni wakiwa na nguvu mpya za kifikra, na kuwa tayari kwa changamoto zinazokuja.
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.