ACT-Wazalendo: Mwili wa Nondo wabainika kuwa na sumu

Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo kimedai madaktari wanaomhudumia  Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Abdul Nondo katika Hospitali ya Aga Khan wamebaini mwili wa kijana huyo kuwa na kiwango kikubwa cha sumu.

Hadi sasa kwa mujibu wa chama hicho, wataalamu hawajafahamu kama sumu hiyo imetokana na athari za kupigwa na kuteswa au alipewa kitu chenye sumu na watekaji wake.

Nondo anapatiwa matibabu Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, baada ya kutekwa na watu wasiofahamika alfajiri ya Desemba 1, 2024 stendi ya mabasi ya Magufuli, Mbezi jijini humo mara baada ya kuwasili akitokea Kigoma kwenye shughuli za kisiasa.

Kwa mujibu wa Nondo watu hao walimfunga mikono kwa kamba na usoni akifungwa kitambaa na kumtesa kwa vipigo maeneo mbalimbali ya mwili wake. Siku hiyohiyo usiku alitekelezwa eneo la Coco Beach na kupata msaada wa bodaboda waliompeleka makao makuu ya chama chake, Magomeni.

Baada ya tukio hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema kuna mtu mmoja mwanaume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari nyeupe lenye usajili wa namba T 249 CMV Land Cruiser. Huku akisema wanaendelea na uchunguzi kubaini waliohusika.

Leo Jumatano, Desemba 4, 2024, Ngome ya vijana wa chama hicho imetoa taarifa kwa umma kuelezea mwenendo wa matibabu ya kiongozi wao. Taarifa hiyo imetolewa na Philibert Macheyeki, Katibu wa Habari na Uenezi wa ngome hiyo.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT- Wazalendo Abdul Nondo akiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kutokana na kuumizwa kwa kipigo na watu wanaodaiwa kumteka.

“Madaktari wamedai mwili wa Abdul Nondo unaonyesha kuwa na kiwango kikubwa cha sumu ambayo mpaka sasa hawajajua kama zimetokana na athari za kupigwa na kuteswa au kama alipewa kitu chenye sumu na watekaji wake.

“Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, umewaomba madaktari kumfanyia uchunguzi zaidi kwa ajili ya kubaini aina ya sumu iliyo mwilini mwake na kama zimetokana na kupewa sumu,” amedai

Macheyeki kupitia taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza: “Kwa sasa hali ya Mwenyekiti Abdul Nondo bado si nzuri, mikono yake imevimba na ana maumivu makali mwilini japo madaktari wanaendelea kupambana kuhakikisha afya yake inaimarika na kurudi kwenye hali yake ya kawaida.”

Juzi, Nondo akizungumzia alivyotekwa, alisema alikuwa anatokea Kigoma na alifika Dar es Salaam, saa 10 alfajiri wakati akitoka nje ya kituo hicho kutafuta usafiri, wakatokea vijana sita, waliomvamia na kumtaka kutopiga kelele.

“Waliniambia nitulie, awali nilihisi ni vibaka, lakini jambo lilikuwa ‘serious’ zaidi baada ya kuona gari nyeupe Hard Top likasogezwa na milango ya nyumba ilifunguliwa ili niingie.

“Nilipiga kelele kuingia katika gari, kuhakikisha siingii, nilikuwa naomba msaada kwa watu waliokuwapo nikawaambia nisaidieni naitwa Abdul Nondo, maana kulikuwa na watu wa boda, wasafiri waliokuwa wanafika kutoka safarini na wengine kwenda mikoani,” alisema Nondo.

Nondo alisema tukio la kutekwa kwake lilikuwa la ghafla, kwa kuwa hakuwa na wazo kama kuna watu wanamfuatilia ili akamatwe.

Alisema ukamataji ule haukuwa wa kawaida kwa sababu waliotekeleza tukio hilo hawakujitambulisha.

“Nilichosikia walikuwa wakilaumu pingu ziko wapi, baada kuzikosa pingu walinifunga kamba kwenye mikono tena kwa nguvu sana mikono ikiwekwa nyuma na usoni walinifunga kitambaa,”amesema.

Katika purukushani za Nondo kuchukuliwa inaelezwa kuwa begi lake lilidondoka huku akisema watu hao wamempa vitisho vya kutoeleza kilichotokea la sivyo watamchukua tena.

Related Posts