Kampuni hiyo yenye kiwanda cha tumbaku mjini Morogoro ilikabidhiwa tuzo ya ushindi huo mwishoni mwa wiki mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja Rasilimaliwatu wa kampuni hiyo, Blasius Lupenza alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa na usimamizi na uongozi mzuri pamoja na wafanyakazi wote kwa kusimamia sera za kampuni na utamaduni wa kufanya kazi.
Alisema, “Kwa niaba ya kampuni tunajivunia sana kusherehekea mafanikio haya bora ya kuwa mshindi wa jumla na pia mshindi kwenye Kitengo cha kuzalisha ajira, kujitolea katika usimamizi wa wafanyakazi, bidi na ari ya ubunifu imeinua kampuni yetu kwenye ukurasa mpya”.
Aliongeza: “Tuzo hizi ni ushuhuda wa mchango wa kipekee na tunashukuru kuwa nao kama sehemu yetu. Tunashukuru ATE kwa kututia moyo”.
Tuzo ya mwajiri bora wa mwaka imejikita katika kuangalia namna taasisi inavyofanya kazi kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo sayansi, taaluma, watendaji wa taasisi, usimamizi wa mashirika katika uwekezaji mdogo na wa kati.
Kwa mwaka huu zaidi ya kampuni na taasisi 100 zilionesha nia ya kushiriki lakini ni 76 pekee zilichaguliwa katika kuwania tuzo hizo zilizogawanywa katika vipengele 10.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amekipongeza ATE kwa kuandaa tuzo ya mwajiri bora wa mwaka na kuwataka washindi kuzingatia viwango vitakavyofanikisha kuendeleza ubora mahali pa kazi.
Dk Biteko alisisitiza kuwa tuzo hizo zinahamasisha ushindani baina ya waajiri na kusaidia kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo usalama kazini, kuongeza viwango vya uzalishaji na kuboresha uhusiano mzuri na wafanyakazi kwa maendeleo ya kampuni na taasisi zao.
“Ninawapongeza ATE kwa kuja na tuzo hizi zitakazosaidia kuboresha mazingira ya kazi na waajiri katika maeneo ya kazi, tunaamini tuzo hizi zitaendelea kuhamasisha ushindani kwa wafanyakazi ili kuendelea kuwa bora zaidi,” alisema.
Tuzo ya mwajiri bora wa mwaka ni moja ya mpango wa ATE unaofanyika kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005 ambapo mwaka huu imetimiza miaka 19.
Lengo la kutoa tuzo hizo ni kuhamasisha nguvu kazi ya pamoja na rasilimaliwatu ili kutekeleza majukumu ya msingi katika uzalishaji na utendeji katika biashara ndani ya kampuni.
Aidha ATE imelenga kuziwezesha taasisi kufanikiwa kutekeleza sera na mipango ya taasisi itakayosaidia kuongeza uzalishaji na ushindani wa kibiashara.
Ofisa Mtendaji mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba alisema tuzo hizo zilianzishwa kwa lengo la kuwatambua waajiri wanaotekeleza mipango madhubuti inayosaidia kusimamia wafanyakazi na biashara kwa ujumla.