ALIYEKUWA kocha mkuu wa Singida Black Stars, Patrick Aussems amemtaja mshambuliaji wa Kenya, Elvis Rupia kuwa mmoja wa washambuliaji hatari katika Ligi Kuu Bara kwa sasa na ana nafasi nzuri ya kuwania kiatu cha ufungaji bora msimu huu.
Aussems ambaye aliiongoza Singida Big Stras katika michezo 11 ikishinda saba, sare mitatu na kupoteza moja dhidi ya Yanga kabla ya kuachana na timu hiyo, alionyesha imani kubwa kwa Rupia.
Mbelgiji huyo ameliambia Mwanaspoti kwamba Rupia ni mchezaji aliye na sifa zote za kuwa mshambuliaji hatari.
“Ana nguvu, kasi na uwezo wa kufunga mabao katika mazingira yote. Ni mchezaji ambaye anaweza kubadilisha mchezo kwa sekunde moja na kwa kiwango alicho nacho sasa ana nafasi kubwa ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora msimu huu,” alisema Aussems.
Rupia ambaye kwa sasa ana mabao matano yupo nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara akitofautiana bao moja na kinara wa mabao, Selemani Mwalimu wa Fountain Gate.
Kwa upande mwingine, Rupia amekuwa akionyesha umahiri kufunga tangu akiwa Ligi Kuu Kenya ambapo aliibuka mfungaji bora msimu wa 2022–23 baada ya kufunga mabao 27 akiitumia Kenya Police.
Mabao hayo yalimfanya Rupia kuvunja rekodi nchini humo baada ya miaka 47 iliyowekwa na Maurice Ochieng aliyefunga mabao 26 katika msimu wa 1976.