CCM Mara yaja kivingine, yatumbukiza Sh860 milioni ujenzi ukumbi wa kisasa

Musoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kinatarajia kutumia zaidi ya Sh860 milioni kwenye ujenzi wa ukumbi wa kisasa utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 2,300 kwa wakati mmoja.

Ukumbi huo ambao umeanza kujengwa mjini Musoma, unatajwa kuwa mkubwa kuliko kumbi zote zilipo mkoani hapa na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mapema mwakani.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Ibrahim Mjanaheri amesema hayo leo Jumatano Desemba 4,2024  mjini hapa na kuongeza kuwa ukumbi huo unatarajiwa kuwa moja ya kitega uchumi cha chama hicho, unajengwa kupitia michango ya wadau mbalimbali.

“Pamoja na kuwa ujenzi unaendelea, bado tuna uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya kuiamirisha mradi huu ambao utekelezaji wake unatokana na maagizo ya chama makao makuu na kamati ya siasa ya mkoa, maagizo ambayo yanalenga kukiimarisha chama kiuchumi, hivyo niwaombe wadau watushike mkono ili mradi wetu ukamilike,” amesema.

Mjanaheri amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa kivutio kikuu kwa mikutano ya kitaifa na kimataifa kufanyika mjini Musoma, ikiwemo mikutano ya kisiasa, kijamii na kiuchumi hivyo kutoa wito kwa wadau kuendelea kuchangia ujenzi wa mradi huo.

Msimamizi wa mradi, Fili Peter amesema mradi huo ulioanza kujengwa Februari 2023,  ulitarajiwa kukamilika Desemba 2024, lakini kutokana na sababu mbalimbali sasa utakamilika mwakani. Mpaka sasa ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 50.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma pamoja na kupongeza uwekezaji huo, wametoa wito kwa wafanyabiashara na mashirika mbalimbali kuwekeza mkoani humo, ikiwa ni pamoja na kujenga kumbi nyingi za kisasa zitakazokidhi mahitaji kulingana na hali ilivyo kwa sasa.

“Kwa sasa tunategemea ukumbi mmoja ambao ndio mkubwa na wenyewe una uwezo wa kuchukua watu si zaidi ya 1,500, kutokana na kukua kwa uchumi na mambo mengine, tuna uhitaji wa kumbi nyingi kubwa na za kisasa, niwaombe wadau watumie fursa hiyo kwani soko lipo la uhakika,” amesema Fazel Janja.

Janja amesema uwepo wa kumbi nyingi kubwa na za kisasa katika  mji wa Musoma na mkoa kwa ujumla utakuwa ni moja ya kichocheo kikubwa cha kufanyika kwa mikutano na matukio makubwa ya kitaifa mkoani humo.

“Nakumbuka kuna mwaka Jumuiya ya Tawala za Mitaa (Alat) walifanya mkutano wao hapa Musoma, kwa kweli hapakuwa na ukumbi wa kutosha kuwachukua wajumbe wote, ilibidi watumie ukumbi ambao ulikuwa bado unaendelea kujengwa ambao kidogo ulikuwa na uwezo wa kuwachukua wajumbe wote,”amesema Derek Maira.

Maira amesema ingawa ukumbi huo unajengwa kama kitega uchumi kwa CCM, lakini una manufaa kwa wakazi wa mji wa Musoma kwani anaamini ukikamilika vikao vya taasisi za umma na binafsi vitafanyika katika eneo hilo, tofauti na ilivyo sasa ambapo vikao hivyo vinafanyika kwenye miji mikubwa kama Mwanza ambako kuna kumbi nyingi na kubwa.

Related Posts