Arusha. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema nchi za Afrika Mashariki (EAC) na za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) zinapaswa kuimarisha teknolojia katika kutekeleza mipango ya nishati bora, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika tafiti na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani.
Aidha, amewahimiza wadau wa maendeleo kuendelea kuchangia uwekezaji katika nishati bora nchini, akisisitiza kuwa nishati hiyo itasaidia kuongeza upatikanaji wa nishati safi na kupunguza matumizi ya nishati duni na utegemezi wa mafuta kutoka nje.
Dk Biteko ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Desemba 4, 2024, jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa kikanda kuhusu matumizi bora ya nishati ukiongozwa na kaulimbiu ‘Kuchagiza matumizi bora ya nishati kwa maendeleo endelevu.’
Amesema nchi za jumuiya hizo zina wajibu wa kuimarisha teknolojia na kutekeleza mipango yake, ikiwemo kuwekeza katika tafiti na wakipata usaidizi wa kifedha katika kutekeleza miradi mikubwa, watakuwa na uhakika wa nishati bora, hali itakayosaidia kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kukuza ukuaji endelevu wa uchumi.
“Utayari wa teknolojia ni nguzo muhimu katika kutekeleza mipango ya ufanisi wa nishati. Tunaweza kufanikisha hili kwa kuwekeza katika tafiti na maendeleo, kushirikiana na wabunifu wa sekta binafsi na taasisi za elimu ili kujenga rasilimali watu yenye ujuzi wa kuendesha teknolojia za kisasa,” amesema.
Amesema licha ya changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo, matumizi bora ya nishati hupunguza gharama za uendeshaji wa biashara hadi ngazi ya kaya ambayo inaweza kuwekezwa katika ukuaji, uvumbuzi na maendeleo ya jamii.
“Kwa kuboresha matumizi bora ya nishati, biashara zinaweza kuongeza tija na kuboresha ushindani na kuzifanya ziwe thabiti zaidi katika soko linalobadilika la kimataifa, itapunguza utegemezi wa mafuta kutoka nje na kupunguza mahitaji ya jumla ya nishati. Hii itasaidia katika usambazaji wa nishati, kulinda uchumi wetu,” ameongeza.
Uzinduzi wa mkakati wa kitaifa
Katika mkutano huo, Dk Biteko amezindua mkakati wa kwanza wa kitaifa wa miaka 10 wa matumizi bora ya nishati.
Mkakati huo utakuwa mwongozo wa kufikia malengo ya ufanisi wa nishati kwa kushirikiana na wadau wote wa maendeleo.
“Tunahitaji kushirikiana ili kupunguza upotevu wa nishati unaokumba nchi nyingi za Afrika. Tafiti zinaonyesha baadhi ya nchi hupoteza hadi asilimia 14 ya nishati yao. Wizara ya Nishati imejipanga kuhakikisha tunafanikisha malengo ya mkakati huu,” amesema.
Uwekezaji wa Benki ya Dunia
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Malawi, Tanzania, Zambia na Zimbabwe, Nathan Belete amesema benki hiyo imewekeza Dola bilioni 9.6 kwa nchi za EAC na SADC, na Tanzania imepata Dola bilioni 1.7. Uwekezaji huo unalenga kusaidia juhudi za Serikali katika upatikanaji, uzalishaji, usambazaji, na ufanisi wa nishati.
“Ufanisi wa nishati ni hitaji muhimu kiuchumi. Katika nchi za SADC, karibu watu milioni 560 wanakosa nishati bora, hali inayorudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi. Nishati bora itapunguza gharama za nishati vijijini na kuboresha shughuli za kiuchumi,” amesema Belete.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba akizunguza katika mkutano huo amesema umeandaliwa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), UNDP na Ubalozi wa Ireland ili kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi bora ya nishati.
“Lengo ni kutafuta njia bora za nchi wanachama kushirikiana katika uandaaji wa viwango na miongozo ya pamoja ya matumizi bora ya nishati. Pia, tunashirikiana na TBS kuhakikisha vifaa vinavyoingia nchini vina ubora wa hali ya juu,” amesema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo, amesisitiza kuwa nishati bora ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi, hasa wakati ambapo ongezeko la idadi ya watu linahitaji nishati endelevu zaidi.