Hapa Fei, pale Ahoua moto utawaka

WAKATI Simba alfajiri ya leo ikiondoka kwenda Algeria, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua ameonekana kumkosha zaidi kocha  Fadlu Davids kutokana na mchango alionao kikosini.

Kiungo huyo aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Stella Club d’Adjamé ya Ivory Coast amechangia mabao tisa kati ya 22 yaliyofungwa na timu yake katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast amecheza mechi 10 kati ya 11 za Simba msimu huu kwa dakika 663.

Ahoua akiwa na mchango huo, naye kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’  amehusika na mabao tisa kati ya 19 ya timu yake ndani ya ligi.

Katika mechi 13 za ligi ambazo Azam imecheza na kukaa kileleni, Fei Toto amecheza zote kwa dakika 1092.

Rekodi za kila mmoja katika mchango wake wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu zinawafanya kuzifunika baadhi ya timu ambazo hazipo vizuri kwenye ufungaji wa mabao.

Katika timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu, saba kati yao zinalingana au kuwa chini ya nyota hao katika takwimu za mabao.

Timu hizo ni JKT Tanzania yenye mabao tisa sawa na KMC, KenGold (8), Pamba Jiji (7), Kagera Sugar (7), Tanzania Prisons (6) na Namungo (5).

Ahoua katika mchango wake wa mabao tisa, amefunga matano na asisti nne, huku Fei Toto akifunga manne na asisti tano.

Ikumbukwe kuwa, msimu uliopita Fei Toto alimaliza na mchango wa mabao 26 akifunga 19 na asisti saba kwenye Ligi Kuu Bara akishika nafasi ya pili kwa ufungaji nyuma ya kinara Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyefunga 21.

Kocha wa Simba, Fadlu David alisema kuwa, Ahoua ni miongoni mwa viungo muhimu katika kikosi chake kwani anamaamuzi sahihi anapokuwa karibu na lango la mpinzani.

“Licha ya namba nzuri alizonazo Ahoua bado ana uwezo wa kufanya vizuri zaidi na ameendelea kudhihirisha  balaa lake kutokana na uchezaji wake wa kasi na wa kutumia nafasi za kufunga,” alisema Fadlu.

Kocha wa Azam, Rachid Touasis akimzungumzia Fei Toto alisema: “Feisal ni mchezaji mzuri na mwenye kipaji kikubwa, anaweza kucheza nafasi nyingi japo ninapendelea kumtumia kama namba 10.

“Namba anayoichezea inamfanya aweze kutumia ubora wake na kutengeneza nafasi, lakini haina maana nimemzuia kufunga, muhimu atengeneze nafasi kwa wenzake na kufunga akiweza.”

Winga wa zamani wa Simba, Uhuru Suleiman, anaamini kuwa mmoja kati ya Fei Toto na Ahoua ana nafasi kubwa ya kuwa mchezaji bora wa msimu ikiwa wataendeleza kiwango chao cha juu kilichoonyeshwa katika raundi hizo.

“Hawa wachezaji wameonekana kuwa na njaa ya ushindi. Fei Toto ameonyesha ufanisi mkubwa, lakini Ahoua naye ameleta mabadiliko makubwa kwa Simba. Ikiwa wataendelea na kasi hii, hakuna ajabu mmoja wao akaibuka mchezaji bora wa msimu,” alisema Uhuru.

Kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina, Mohamed Badru, alisema: “Huwa si jambo la kushangaza kuona Fei Toto na Ahoua wakiwa kwenye kilele cha ubora huu. Wote wanacheza kwa ustadi mkubwa, na kama wataendeleza kiwango hiki, watafanya mapinduzi makubwa katika ligi hii.

“Fei Toto ni mchezaji ambaye ana uwezo wa kubadilisha mchezo muda wowote, na Ahoua amewapa Simba kitu kipya. Huu ni msimu wa wachezaji hawa na hakuna kinachowazuia.”

Related Posts