Hofu kukosekana kwa vijana yatajwa kuchochea maambukizi VVU

Mwanza. Kutokuwa na hofu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na changamoto za maisha, zimetajwa kuwa sababu kuu zinazochangia ongezeko la maambukizi mkoani Mwanza, kutoka asilimia 16 hadi asilimia 28 kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24 kati ya mwaka 2022 na 2023.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022/2023, kiwango cha jumla cha maambukizi ya VVU mkoani Mwanza kilishuka kutoka asilimia 7.2 hadi asilimia 4.7.

Pia, kumekuwepo na ongezeko la maambukizi miongoni mwa vijana wa rika balehe, hali inayotajwa kuchangiwa na sababu mbalimbali kama ugumu wa maisha, tamaa, malezi duni na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu VVU.

Baadhi ya vijana waliozungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano, Desema 4, 2024 wamesema hofu juu ya Ukimwi imepungua kutokana na mtazamo kuwa ugonjwa huo si tishio tena.

Fatuma Ally, mkazi wa Kata ya Pamba jijini Mwanza, amesema watu wameamua kupuuzia Ukimwi kwa sababu hauogopeshi tena.

“Kwa mfano, vijana wanaogopa zaidi magonjwa kama UTI, saratani na fangasi kuliko Ukimwi,” amesema Fatuma.

Kwa upande wake, Juma Ramadhani, mkazi wa Kata ya Butimba amesema upatikanaji wa dawa za kufubaza virusi (ARV) umewafanya vijana wengi kupuuza athari za VVU kwa miaka ya hivi karibuni.
“Siku hizi vijana wanaona Ukimwi si tatizo kubwa kwa sababu ARV zinawasaidia kuendelea kuishi maisha ya kawaida. Wanaogopa zaidi kupata mimba kuliko maambukizi ya VVU,” anasema Juma.

Kwa upande wake, muelimishaji rika wa Shirika la ICUP wilayani Misungwi, Jenipher Bamusiba ametaja utandawazi, tamaa na ugumu wa maisha kuwa sababu kuu zinazowasukuma vijana kujihusisha na biashara ya ngono.

Amesema baadhi ya vijana hufanya hivyo ili kupata fedha za kukidhi mahitaji kama kununua simu au mavazi.

Pia amesema malezi duni, hususan kwa watoto wanaolelewa na wazazi wa umri mkubwa au mzazi mmoja, yanachangia tabia hatarishi.

Miriam Nkwabi, wa Shirika la Wanawake na Wasichana wanaoishi na VVU (DWWT) amebainisha kuwa vijana wengi wa rika balehe hawana elimu ya kutosha kuhusu maambukizi ya VVU.

Ametoa wito kwa Serikali kuongeza juhudi za utoaji elimu, ili kuliokoa kundi hilo lililo hatarini zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ludigila amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wadau na jamii katika kutoa elimu na malezi bora kwa vijana.

“Nitoe rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatoa malezi sahihi na elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU ili kufanikisha lengo la Taifa la 95-95-95,” amesema Ludigila.

Related Posts