Huyu ndiye Nandi-Ndaitwah, Rais mteule wa Namibia

Ndemupelila Netumbo Nandi-Ndaitwah, anatarajiwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Namibia na wa kwanza mwanamke katika nchi hiyo, baada ya kushinda kwenye uchaguzi mkuu kwa kupata asilimia 57.

Amemshinda mpinzani wake, Panduleni Itula wa IPC aliyepata asilimia 26 ya kura zote.

Mshindi huyo ameendeleza utawala wa chama cha Swapo kilichopigania uhuru wa nchi hiyo na kuwezesha kupata uhuru mwaka 1990 kutoka kwa utawala uliokuwa makaburu wa Afrika Kusini.

Kabla ya kugombea nafasi hiyo, Nandi-Ndaitwah alikuwa makamu wa tatu wa rais wa Namibia tangu Februari 2024. Mwaka 2017, alichaguliwa kuwa makamu wa rais wa Swapo, mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.

Netumbo Nandi alizaliwa Oktoba 29, 1952 huko Onamutai, Ovamboland, Afrika ya Kusini Magharibi (ambayo leo ni Mkoa wa Ohangwena, kaskazini mwa Namibia). Baba yake alikuwa kasisi wa Kanisa la Anglikana.

Ni mtoto wa tisa kati ya watoto 13 wa familia yao, alipata elimu yake ya awali katika Misheni ya Mtakatifu Maria huko Odibo.

Mwaka 1974, alikimbilia uhamishoni na kujiunga na wanachama wa Swapo nchini Zambia. Alifanya kazi katika makao makuu ya Swapo huko Lusaka kutoka 1974 hadi 1975 na akahudhuria kozi katika Shule ya Lenin Higher Komsomol nchini Umoja wa Kisovyeti (USSR) kuanzia 1975 hadi 1976. Alipata diploma katika kazi na mazoea ya harakati za vijana wa Kikomunisti.

Mwaka 1987, alipata stashahada ya uzamili katika usimamizi na utawala wa umma kutoka Chuo cha Teknolojia cha Glasgow, Uingereza. Mwaka 1988, alipata stashahada ya uzamili katika uhusiano ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Keele, pia nchini Uingereza.

Mwaka mmoja baadaye, 1989, Nandi-Ndaitwah alihitimu shahada ya uzamili katika masomo ya kidiplomasia kutoka Chuo Kikuu cha Keele.

Aliteuliwa kuwa mwakilishi msaidizi wa Swapo nchini Zambia kuanzia mwaka 1976 hadi 1978 na baadaye mwakilishi mkuu wa chama hicho nchini Zambia kutoka 1978 hadi 1980. Kuanzia mwaka 1980 hadi 1986, alihudumu kama mwakilishi mkuu wa Swapo katika Afrika Mashariki makao yake yakiwa Dar es Salaam, Tanzania.

Alikuwa pia mwanachama wa kamati kuu ya Swapo kuanzia 1976 hadi 1986 na rais wa Shirika la Kitaifa la Wanawake wa Namibia (Nanawo) kuanzia 1991 hadi 1994.

Nandi-Ndaitwah amekuwa mbunge tangu mwaka 1990. Kuanzia 1990 hadi 1996, alihudumu kama Naibu Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano. Mwaka 1996, alipata hadhi ya uwaziri kwa mara ya kwanza alipoteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa masuala ya wanawake katika Ofisi ya Rais, nafasi aliyoshikilia hadi mwaka 2000. Mwaka huohuo, alipandishwa cheo kuwa waziri kamili na kupewa wizara ya Masuala ya Wanawake na Ustawi wa Watoto.

Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Netumbo Nandi-Ndaitwah alikuwa Waziri wa Habari na Utangazaji katika baraza la mawaziri la Namibia. Baadaye alihudumu kama Waziri wa Mazingira na Utalii hadi mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri Desemba 2012, na aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, nafasi ambayo baadaye ilibadilishwa jina kuwa Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano.

Chini ya Rais Hage Geingob, Nandi-Ndaitwah aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Namibia Machi 2015, huku akiendelea kuhudumu kama Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano.

Nandi-Ndaitwah ni mwanachama wa kamati kuu ya Swapo na politburo ya chama hicho. Pia ni katibu wa habari na uhamasishaji wa Swapo, na hivyo ni miongoni mwa wasemaji wakuu wa chama hicho.

Machi 2023, hayati Rais Hage Geingob alimtangaza Netumbo Nandi-Ndaitwah kuwa mgombea urais wa chama cha Swapo katika uchaguzi mkuu wa Namibia wa mwaka 2024.

Baada ya kifo cha rais huyo, Geingob Februari 2024, Nandi-Ndaitwah aliteuliwa kuwa makamu wa rais, akichukua nafasi ya Nangolo Mbumba aliyekaimu nafasi ya urais.

Related Posts