Iringa wachekelea huduma za madaktari bingwa 56

Iringa. Siku chache baada ya kuanza kwa kambi ya kanda yakKati ya madaktari bingwa 56 wanaojulikana kama ‘madaktari wa Samia’ katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, wananchi waliopata huduma wameelezea furaha yao.

Kambi hiyo iliyoanza juzi, itadumu kwa siku tano. Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano, Desemba 4, 2024, baadhi ya wagonjwa wamesema huduma hizo zimekuwa mkombozi mkubwa kwao, hasa ikizingatiwa gharama kubwa na umbali wa kuzifuata katika mazingira ya kawaida.

Mgonjwa mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake, mkazi wa Kihesa, amesema kwa miaka mitatu sasa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya hedhi ya mara kwa mara na nyingi.

“Niliposikia kuna madaktari bingwa wamefika Iringa, nilikwenda kupima na nikagundulika kuwa nina uvimbe tumboni. Sasa ninasubiri kufanyiwa upasuaji,” amesema mkazi huyo.

Amesema anaishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma hizo za kibingwa kwa kuwa wagonjwa wengi wanashindwa kuzifikia kutokana na gharama na umbali.

Faridah Ignas, mkazi wa Frelimo katika Manispaa ya Iringa, naye ametoa ushuhuda kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa uvimbe wa mayoma uliomsumbua kwa muda mrefu, sasa anajisikia vizuri.
“Nilihitaji damu kabla ya upasuaji na madaktari walihakikisha napata huduma hiyo. Nashukuru sana madaktari bingwa kwa huduma bora walizonipa,” amesema Faridah.

Amesema awali alimbiwa anahitaji kuonana na dktari bingwa, lakini kutokana na ugumu wa maisha alishindwa kupata tiba kutokana na kukosa fedha.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea, zaidi ya wagonjwa 800 wamehudumiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Iringa tangu kambi hiyo ianze, huku zaidi ya wagonjwa 4,000 wakihudumiwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa huduma za kibingwa zinazotolewa zinajumuisha vipimo, dawa na upasuaji mkubwa kwa wagonjwa waliopangiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, alizindua rasmi kambi hiyo ambayo inahusisha mikoa ya Iringa, Singida, Morogoro, Dodoma na Pwani.

Kambi hiyo inatarajiwa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 5,000 ndani ya siku tano, huku zaidi ya wagonjwa 1,000 wakipangiwa upasuaji mkubwa.

Related Posts