Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku 16 za kupinga ukatili, kundi la watoto wa kiume limetajwa kuwa hatarini kukumbwa na majanga ya ukatili ukiwemo ulawiti na kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Lakini wengine wanatajwa kujiunga na makundi ya uhalifu kama uporaji, ujambazi na watumiaji wakubwa wa dawa za kulevya.
Kila mwaka hufanyika kampeni maalumu ya kuzuia ukatili katika Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka na mara nyingi imekuwa ikiwalenga wanawake na watoto wa kike kwa kiwango kikubwa.
Na ndani ya siku hizi, kumekuwa na mikakati mbalimbali ikitajwa ya namna ya kuwawezesha watoto wa kike kimalezi, kielimu, maeneo ya kazi na katika uongozi.
Kampeni hizo zinajengwa katika msingi kuwa wanawake wako nyuma kielimu na kiuongozi na kwamba, wako kwenye kundi lililo hatarini katika unyanyasaji wa kingoni na ukatili wa maungoni.
Wakati kampeni hizo zikiendelea, kumekuwa na hofu kuwa watoto wa kiume nao hivi sasa wameachwa kimalezi kiasi cha kuwa hatarini kutumbukia kwenye uhalifu na ukatili.
Mwanasaikolojia Jacob Kilimba anasema tatizo la kutowajumuisha watoto wa kiume katika malezi limekuwa na mizizi ya kihistoria, hasa katika kipindi cha miaka ya 1990 hadi 2000. Katika kipindi hiki, anasema juhudi kubwa zilielekezwa kuwawezesha watoto wa kike kutokana na changamoto walizokuwa wakikumbana nazo, kama kutengwa katika elimu na kutopata fursa za ajira.
“Matokeo yake, kulisahaulika kumwandaa mtoto wa kiume kukabiliana na maisha,” anasema Kilimba alipokuwa akizungumza na Mwananchi kuhusu kampeni hiyo inayolenga suala hili.
Anaongeza kuwa hali hiyo imewafanya wanaume wengi kushindwa kuishi na wanawake walioelimika ndani ya ndoa.
“Mtoto wa kiume hakuandaliwa vya kutosha kuhusiana na jukumu la kuilea familia. Hali hii inasababisha migogoro ya mara kwa mara ndani ya ndoa na mara wanapoachana, watoto wanakosa malezi ya baba. Hii ni kwa sababu baba anapaswa kuwa na mchango unaoonekana wazi, hata katika masuala ya kifedha,” amesema.
Kilimba pia anabainisha kuwa watoto wa kiume mara nyingi hutengwa kihisia ndani ya familia, hasa pale baba anakuwa hayupo na maswali yao ya kihisia hayapatiwi majibu stahiki na mama.
Hata hivyo, licha ya kwamba takwimu zinaonyesha wanawake bado wako nyuma katika nyanja za elimu, ajira na uongozi, wadau mbalimbali wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kutowasahau watoto wa kiume.
Mkurugenzi wa Programu wa Chama cha Uzazi na Malezi Bora (Umati), Daniel Kirhima anasema licha ya juhudi za kuwawezesha watoto wa kike, wanajitahidi pia kuwahusisha watoto wa kiume.
“Sisi Umati tunashirikisha watoto wa kiume kwa sababu tunatambua mchango wao katika kusaidia watoto wa kike. Kupitia programu zetu, tuna vipengele maalum vya kuwahusisha wanaume na midahalo inayolenga kuwaandaa watoto wa kiume kwa majukumu ya uzazi na malezi,” anasema Kirhima.
Ameongeza kuwa hata katika kampeni za kupinga mimba za utotoni, wanawashirikisha watoto wa kiume, kwa kuwa nao ni wadau muhimu wa pili katika changamoto hizo.
“Mradi unaweza kuwa unalenga watoto wa kike, lakini tunawajumuisha pia watoto wa kiume kwa sababu wanahusika moja kwa moja,” amesisitiza.
Wito wa kuhakikisha watoto wa kiume hawapuuzwi katika malezi na maendeleo umekuwa ukitolewa na viongozi na wadau mbalimbali nchini.
Akizungumza Aprili 7, 2024, wakati wa uzinduzi wa taasisi ya Safari ya Mwanamke Foundation inayotoa msaada wa kisheria kwa wanawake, mwanasiasa huyo alisema: “Tukiwapoteza vijana wa kiume, tutakuwa na changamoto kubwa, maana hata hawa watoto wa kike tunaowasaidia watakumbana na matatizo kwa kuwa wataolewa na wanaume wasiojielewa.”
Mongella ambaye ni mwanaharakati wa haki za wanawake na mshiriki wa mkutano wa kihistoria wa Beijing uliofanyika China mwaka 1995, alisisitiza kuwa wanawake ni mama wa vijana wa kiume na kwa msingi huo, juhudi kubwa zinahitajika pia katika kuwawezesha na kuwalea vijana wa kiume kwa uangalifu.
Mwaka huu pia ulishuhudia kilio cha baadhi ya wabunge kuhusu haja ya kuwakumbuka watoto wa kiume katika mpango wa Serikali wakati wakichangia hotuba ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia wanawake na Makundi Maalum kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza katika mjadala huo Mei 17, 2024, Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu alimtaka Waziri Dorothy Gwajima ajibu kuhusu mipango ya Serikali na mtoto wa kiume.
“Leo mimi nasimama hapa, naomba rasmi, kama tunapitisha hii bajeti ya Maendeleo ya Jamii, namwomba Waziri atakaposimama atujibu haya ipasavyo, vinginevyo nimwombe mheshimiwa Rais kwa heshima na taadhima, atupe wizara nyingine ya jinsia ya kiume kwenye nchi hii.
“Namna tunavyokwenda hakuna usawa katika kuzingatia makundi katika nchi yetu, wanaume wanaachwa, watoto wa kiume wanaachwa na hawa ndio wako kwenyesehemu ya risk (hatari).
Akisoma vipaumbele vya wizara hiyo, Msambatavangu alisema katika kuratibu afua za kukuza usawa wa kijisia uwezeshaji wanawake kiuchumi na utekelezaji wa Mpango kazi wa Kitaifa wa kutokomeza ukatili wa wanawake na watoto, wanaume hawamo.
“Katika eneo la kukuza usawa wa kijinsia uwezeshaji wa wanawake kiuchumi anawatengea wanawake Sh3.2 bilioni, wanaume hawamo.
“Katika eneo la kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, wanaume hawamo na amewatengea Sh3.15 bilioni, wanaume hawamo,” alisema.
Akizungumzia majukumu ya wizara hiyo yaliyoelezwa katika fungu 53 la hotuba hiyo, Msambatavangu alisema pia hayaelezi mikakati ya kuwasaidia wanaume.
“Ndio maana ninaomba leo hapa tupewe wizara ya wanaume, hatuwezi kupambana na hivi vitendo kwa kwenda bila kuwashirikisha baba zao, au bila kuwashirikisha ambao pia huwa wanahusika kwa namna moja au nyingine.
Aliendelea kueleza kuwa, licha ya tathmini iliyofanywa Oktoba 2022 kuonyesha kupungua kwa ukatili wa kimwili kwa wanawake kutoka asilimia 40 mwaka 2015 asilimia 20 mwaka 2022 kwa wanawake, wanaume hawatajwi.
“Unataka kuwawezesha wanawake kiuchumi sawa, unapowaacha wanaume wakiwa masikini wanaume wataishi vipi? Hawa vijana wetu leo tusipoweka mipango ya kuwawezesha watakapokuwa wanahitaji kuoa ili matamanio yao ya ngono yaishie kwa wake zao wataoa kwa kutumia nini?” alihoji.
Akijibu hoja za wabunge Mei 17, 2024, Waziri Dk Gwajima alisisitiza kuwa amezingatia na hata Mbunge wa Arumeru Magharibi, Noah Saputu alipomtaka Waziri aonyeshe masikitiko na uzito kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanaume na wanawake ameangua, aliangua ‘kilio’ wakati akimjimbu.
Waliwahi kulilia watoto wa kiume
Kilio kama hicho pia kiliwahi kutolewa bungeni Februari 2, 2023 na Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga, akisema jamii imemsahau mtoto wa kiume.
“Tumesahau kabisa malezi ya watoto wa kiume. Watoto wa kiume wamekuwa kama kuku huria, wanajichungia tu hawana mtu wa kuangalia.
“Mambo mengi sasa hivi tunayofanya tunamwangalia mtoto wa kike tu, tumesahau kabisa kwamba mtoto wa kiume ni sehemu ya familia,” amesema.
Alionya kwamba Taifa linaandaa bomu ambalo litakuwa gumu kulidhibiti.
“Angalia watoto wa panyarodi sasa hivi, hakuna panyarodi wa kike, ni wa kiume kwa sababu wamesahaulika na jamii na sasa tunatengeneza bomu kubwa. Naitaka Serikali kuja na mkakati wa kumrudia mtoto wa kiume,” alisema.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko alimpa taarifa Mtinga akisema bado watoto wako nyuma na mikakati iliyopo inalenga kuwasogeza walipo wa kiume.
“Kiuhalisia, mtoto wa kike alikuwa ameachwa mbali sana, hata ukiangalia makazini uwiano wa wanaume na wanawake bado ni ndogo sana, hata ukiangalia mchanganuo wa mawaziri wa kiume na wanawake bado wako mbali sana,” alisema.
Naye Spika Dk Tulia Ackson aliongezea hoja hiyo akisema hata takwimu bado zinaonyesha kuwa mtoto wa kike yuko nyuma.
“Angalia hatya humu ndani, wabunge wanawake wako wangapi asilimia yao? Wabunge wa kiume mko asilimia ngapi?” alihoji.
Mwaka huo huo pia, Spika mstaafu, Job Ndugai alisisitiza haja ya jamii kutomsahau mtoto wa kiume.
Akizungumza katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dodoma, Desemba 21, 2023, Ndugai alisema tangu juhudi za kuwawezesha wanawake ziliposhika kasi, upande wa pili umesahaulika.
“Mtakumbuka kwamba tangu Beijing (mkutano wa wanawake uliofanyika jijini Beijing China mwaka 1995), tumejishughulisha sana na mtoto wa kike na tukajishughulisha na mwanamke,” alisema.
Alisema licha ya matokeo mazuri ya juhudi hizo, lakini kumezaliwa tatizo lingine kwa watoto wa kiume.
“Ninachosema sisi kama jamii tumemwacha mtoto wa kiume wamekuwa ni chokoraa, panyarodi, dawa za kulevya, Magereza wengi ni wao.
“Ukiwalinganisha watoto wa kiume na kike, hata ukiwatembelea shuleni mwalimu akawaruhusu, utawaona wa kiume wanarudi nyuma, watoto wa kike ndio wanakuja mbele.