Je, Tanzania inaandika rekodi ya utekaji, mauaji?

Tumshukuru Mungu kwa Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo kupatikana akiwa hai, japo amejeruhiwa. Tena vibaya, kama ilivyotaarifiwa. Inaumiza, lakini afadhali.

Wengine hatujui walipo. Tutawaona tena au ndiyo kimya milele? Watekaji wanajua. Mungu anajua. Inawezekana wakiona tunaulizia walipo ndugu waliopotea kwa muda mrefu, watekaji wanacheka. Wanaona tunajisumbua bure. Wao wanaujua ukweli.

Lazima tufahamu na tukubaliane kwa kauli moja kuwa hali ni mbaya. Utekaji, ukamataji kwa nguvu, upotezaji watu, imegeuka fasheni. Naam, fasheni ya Tanzania ya kisasa. Inalazimishwa tuone kawaida. Mtu anapotea, yanapigwa mayowe, kisha kinafuata kimya. Anasakwa mwingine wa kupotezwa. Huo ndiyo mzunguko.

Swali; hii fasheni mpya ya Tanzania ya kisasa uelekeo wake ni upi? Watanzania waendelee kunyakuliwa kama vifaranga vya kuku uwanjani dhidi ya mwewe mwenye njaa? Mpaka lini? Inaonekana watekaji au wapoteza watu ni kikundi au mtandao wenye nguvu sana. Polisi huona giza kila wanapofanya uchunguzi.

Hatari na mazingira yanayoweza kukatisha tamaa, Jeshi la Polisi Tanzania, limekuwa katikati ya tuhuma za matukio ya utekaji. Mathalan, viongozi wa ACT-Wazalendo, walitoa taarifa kuwa Nondo alifichwa Kituo cha Polisi Gogoni, Kibamba, Dar es Salaam.

Viongozi wa ACT-Wazalendo pia walitoa taarifa kuwa gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop, lenye namba za usajili T249 CMV, lilikutwa Kituo cha Polisi Gogoni, likiwa linabadilishwa namba za usajili. Gari hilo linatajwa kuwa ndilo lililotumiwa na watekaji kuondoka na Nondo baada ya kumteka Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi, Dar es Salaam.

Taarifa ya msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime ilijibu madai hayo kuwa gari, Toyota Land Cruiser Hardtop, lililokutwa Kituo cha Polisi Gogoni, silo lililotumika kumchukua Nondo Kituo cha Mabasi cha Magufuli. Nondo alipanda basi Novemba 30, 2024, mkoani Kigoma. Alifika Dar es Salaam (Kituo cha Magufuli), Desemba Mosi, 2024, saa 10 usiku.

Mashuhuda walisema watekaji walidondosha pingu wakati wa purukushani za kumchukua Nondo. Kwa wengine, hiyo ni alama kuwa polisi ndio waliohusika. Wapo wanaoona pingu siyo kigezo cha kuthibitisha kwamba wahusika ni polisi. Pengine watekaji hubeba pingu ili kujenga uhusiano baina ya matukio yao na Jeshi la Polisi.

Nilisikiliza mahojiano baina ya Nondo na mtangazaji Rashid Chilumba wa idhaa ya Kiswahili ya DW, Ujerumani. Alisimulia kuwa watekaji walisema yeye (Nondo) ni kidomodomo, ndiyo maana walimshughulikia. Nondo ni mkosoaji wa Serikali. Inawezekana watekaji wanataka kujenga tafsiri kuwa wanaoteka ni serikali?

Macho na masikio ni kwa Nondo leo. Miezi minne kabla, walitekwa vijana watatu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Wilaya ya Temekee, Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise. Kimya mpaka leo.

Septemba 7, 2024, mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao, alichukuliwa na watu wasiojulikana, alipokuwa kwenye basi, akisafiri kutokea Dar es Salaam kwenda Tanga. Kibao, alishushwa akiwa eneo la Tegeta, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Septemba 8, 2024, Jumapili, Kibao, alikutwa ameuawa na mwili wake kumwagiwa tindikali, hasa sehemu ya usoni.

Wapo wanaoamini kwamba kama siyo viongozi wa ACT-Wazalendo kutoa taarifa haraka, ikiwemo namba za gari kutambuliwa na kusisitiza kuwa Nondo alifichwa Kituo cha Polisi Gogoni, pengine ingekuwa hadithi kama ya Soka, Mbise na Mlay, mpaka leo haijulikani walipo. Inawezekana hadithi ya Kibao ingejirudia.

Ni Tanzania mpya. Alipopotea kada wa Chadema, Ben Saanane miaka minane iliyopita, ilikuwa mshangao kwa nchi. Wakafuata, mwandishi wa habari, Azory Gwanda na mwanasiasa Simon Kanguye. Hivi sasa imekuwa kama kawaida. Mithili ya mwewe mwenye njaa kwenye uwanja wenye vifaranga vya kuku visivyo na ulinzi.

Waziri wa Mambo ya Ndani mmoja hadi mwingine. Mwigulu Nchemba kisha Kangi Lugola. George Simbachawene hadi Hamad Masauni, hali ni ileile. Tena, matukio yanaongezeka na kutisha zaidi.

Ni ishara kuwa suluhu ya utekaji imekosekana kadiri mawaziri wanapobadilishwa.

Kutoka Dk John Magufuli mpaka Rais, Samia Suluhu Hassan, tiba ya utekaji imeshindikana bila shaka.

Kwa jinsi matukio haya yanavyozidi utokea huenda ni kielelezo kuwa utekaji ni fasheni mpya ya Tanzania.

Jinsi Tanzania inavyoandika rekodi ya matukio ya utekaji na uhalifu mwingine wa mashambulizi na mauaji, bila kusahau shambulizi la risasi nyingi alilofanyiwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, Septemba 7, 2017, mshangao ni jinsi upelelezi unavyokwama.

Wahusika hawajulikani, hawakamatiki.

Related Posts