Unguja. Serikali imesema kumeibuka wimbi la matumizi mabaya ya fedha (noti) katika shughuli za kijamii, hususani kwenye sherehe za harusi ambako watu hutunza wahusika kwa kuwarushia, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Pia noti hizo huviringishwa kwenye maumbo mbalimbali na kutumika kama mapambo ambayo huvishwa mwili wa mtu ulioloa jasho na matukio mengine yanayofanana na hayo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Makungu Juma Makungu amesema hayo leo Jumatano, Desemba 4, 2024 katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Zanzibar.
Makungu alikuwa akijibu swali la mwakilishi wa Kwerekweke, Ameir Abdalla Ameir aliyetaka kujua matumizi haramu ya fedha ya Kitanzania na hatua gani za kinidhamu zinaweza kutumika kwa mwananchi anayeidhalilisha na kuitoa thamani fedha halali ya Kitanzania.
Makungu amesema katika maeneo ya starehe kumeibuka tabia ya kudhalilisha fedha hizo kwa kuzitupa, kuziviringisha na kutengeneza maua na wakati mwingine noti zinaanguka sakafuni na kukanyagwa.
“Matendo haya yanatweza fedha ya Tanzania ambayo ni moja ya tunu za Taifa letu. Vitendo hivyo vinaendelea kutokea licha ya Benki Kuu ya Tanzania na viongozi mbalimbali wa Serikali kwa nyakati tofauti kuvikemea.
“Serikali inapenda kuufahamisha umma kwamba, kuharibu noti au sarafu, au kuonyesha dharau au dhihaka kwa noti au sarafu za Jamhuri ya Muungano ni kosa la jinai,” amesema.
Hiyo ni kwa mujibu wa kifungu namba 332A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyorejewa mwaka 2002.
Amesema mwananchi yeyote atakayetenda kosa hilo kwa makusudi anaweza kushtakiwa kwa kosa la jinai kwa kupewa adhabu ya faini au kifungo.
Waziri Makungu amesema kama kosa limefanywa na mtumishi wa umma, mtumishi huyo anaweza kupata adhabu ya kinidhamu kama vile kufukuzwa kazi au kuondolewa katika nafasi yake.
Ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha wananchi kutojihusisha na vitendo vya aina hiyo, endapo ikibainika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika.
“Serikali inatoa rai kwa wananchi kuzitunza fedha zetu kwa kuwa ni mojawapo ya tunu na alama muhimu ya uchumi wa nchi yetu. Vilevile, utunzaji mzuri wa fedha zetu utapunguza uwezekano wa fedha hizo kuchakaa mapema na kupunguza gharama za uchapishaji,” amesema.