Kwanini muhimu mzazi kushiriki vikao vya Shule

Dar/mikoani. Kipi kinakuja kichwani unapopokea barua au wito wa wazazi kushiriki kikao katika shule anayosoma mwanao?

Majibu ya swali hilo, yanaakisi mitazamo ya wazazi wengi ambao kwao wanachukulia wito wa vikao hivyo kama mbinu za walimu kutengeneza mtaji wa kuvuna fedha kutoka kwa wazazi.

Kwa mujibu wa baadhi ya walimu wanaeleza mitazamo hasi ndiyo inayosababisha mahudhurio duni ya wazazi katika vikao hivyo ambavyo kimsingi ni njia nzuri ya ushirikishwaji kwa maendeleo ya shule na wanafunzi kwa ujumla.

Ingawa baadhi ya wazazi wana mitazamo hiyo, suala la vikao vya wazazi shuleni limehalalishwa na Sheria ya Elimu Na 25 ya mwaka 1978, inayotaka shule za sekondari kuwa na bodi za shule, huku za msingi kuwa na kamati.

Hatua ya kuhalalishwa na kisheria inaonyesha umuhimu wa vikao hivyo vinavyojadili masuala muhimu kama taaluma, nidhamu na miundombinu.

Hoja ya umuhimu wa vikao hivyo inapigiliwa msumari na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mutahabwa anayesema vinatoa nafasi ya jamii kushiriki katika maendeleo ya shule kwa ujumla.

“Kwa sababu shule ipo kusaidia jamii, lazima ijulikane kama ina changamoto na inatakiwa kuendeshwaje na ndiyo maana tunahimiza ushirikishwaji wa jamii,” anasema.

Hatua ya shule kuendeshwa vikao, anasema inavunja sera ya elimu inayotaka jamii ishiriki kikamilifu katika maendeleo ya elimu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, mkoani Kilimanjaro, Laurence Kisima anasema vikao hivyo husaidia kuweka mipango ya shule kwa pamoja.

“Vikao vya wazazi kwangu vina mwitikio mkubwa, kwa mwaka tunaweza kuwa na vikao vitatu au vinne na ushirki wao unatusaidia kujadili mipango mbalimbali ya shule na maendeleo ya shule kwa pamoja,” anasema.

Kwa sababu ya vikao hivyo, anasema shule hiyo awali haikuwa na matundu ya vyoo na madarasa ya kutosha lakini wameshirikiana na wazazi vimepatikana.

Pamoja na mambo mengine, amesema vikao hivyo pia vinapunguza mikwaruzano baina yao na wazazi pale panapojitokeza changamoto ya wanafunzi kufanya vibaya.

Katika mahudhurio ya vikao vya wazazi yanatofautiana kati ya shule za Serikali ambazo wazazi hawahudhurii na shule binafsi ambazo wanafika japokuwa si wote.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buyegu ya Mwanza ambayo ni binafsi, Malimi Malimi amesema kwa mwaka shule hiyo hufanya vikao viwili na wazazi, na zaidi ya asilimia 85 ya wazazi wanahudhuria.

“Kwenye kikao tunajaribu kuwaeleza zile kero tunazoziona kwa watoto hasa wale wazazi ambao hawawasimamii vizuri pia wazazi wanatumia vikao hivyo kutoa maoni na kushauri shule kwenye mambo fulani ambayo wanaona mtoto hajatendewa haki,” amesema Malimi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Sengerema ya jijini Mwanza, Zakaria Kahema amesema ingawa wanafanya vikao viwili kwa mwaka, mwitikio wa wazazi ni mdogo hivyo kufanya wachache kueleza changamoto na maamuzi kwa niaba ya wengine.

“Kati ya wazazi wa wanafunzi zaidi ya 500 ni wazazi 100 pekee ndio mara nyingi huudhuria vikao vya shule sababu kubwa ni umbali wa maeneo wanayotokea kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanatokea nje ya mkoa wa Mwanza.

Mkazi Mbeya, Silvia Kisare ambaye mtoto wake anasoma shule ya sekondari binafsi anasema ni muhimu kushiriki vikao hivyo ili kusikiliza matatizo na mikakati ya shule.

“Ada ni Sh1.8 milioni kwa mwaka lazima niwe na uchungu nayo ndio maana kila kikao nashiriki ili kufuatilia maendeleo ya watoto na kujua ada inavyotumika, maana nikifika napata fursa ya kukutana na mwalimu wa somo linalomsumbua mtoto na kujua sababu na nini kinafanyika,” amesema Silvia.

Changamoto zinazojitokeza

Mzazi James Mwanda amesema baadhi yao hupuuzia vikao kwa kutopewa nafasi ya kushauri na hata wakipewa fursa hiyo mawazo yao hupuuzwa bila kufanyiwa kazi.

“Ukiomba kushauri wanakuona unapinga kila kitu na wakikupa nafasi kile unachoshauri hakitekelezwi maana yake wanakuwa wameshapanga yao sisi tunaenda kama ushahidi na kuhalalisha idadi ya wazazi,” amesema Mwanda.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bidii mkoani Mwanza, Lugiko Mhuli amesema sababu ya baadhi ya wazazi kutohudhuria vikao ni matokeo na mwenendo wa watoto wao kitaaluma, shughuli nyingi za kikazi na utoaji wa ratiba ya vikao.

“Kuna wazazi wanataka watoto wafanye vizuri kila wakati, lakini inabidi tuangalie pia hali ya mtoto kisaikolojia hivyo wanapokuja kwenye vikao tukiongelea hilo wanarudi kuwaadhibu watoto na kususia vikao,” amesema Mhuli.

Mwalimu Julius Mtui wa Moshi amesema wanahitaji kujadili malezi na makuzi ya mwanafunzi lakini baadhi ya wazazi wanafika wakiwa tayari wamelewa.

“Changamoto nyingine ni pale ambapo wazazi wanapokuja kwenye vikao wakiwa wamelewa, wakati mwingine hawataki kuelewa mambo ya maendeleo yanayopangwa, hivyo mwisho wa siku inakuwa ni changamoto,” amesema Mtui.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi iliyopo Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, Peter John amesema wapo wazazi wanaoamini vikao hivyo ni kwa ajili ya kutozwa fedha.

“Mzazi ameshaitwa kwenye vikao mara kadhaa hata kama linamhusu mtoto wake majibu wanayotoa walimu wanataka pesa wakati Serikali imesema elimu bure,” amesema John.

Akisisitiza umuhimu wa vikao, Kamishna wa Elimu, Dk Mutahabwa amesema mtoto siyo gunia, anapaswa kufuatiliwa wakati wote.

“Nawaambia watu hakuna rasilimali muhimu kama mtoto na kama hakuna hilo utamuangalia mtoto kufa na kupona na moja wapo ni kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya mzazi na shule inayokulelea lulu yako,” amesema.

Amesema hakuna cha muhimu ambacho anakuwa nacho mzazi kama si mtoto.

Amewasihi wazazi kujenga tabia ya kuwa karibu na shule ili kwa pamoja wawalee watoto.

Ili kukabiliana na changamoto ya wazazi kutohudhuria kwenye vikao baadhi ya kamati za shule za msingi nchini ikiwepo jijini Dar es Salaam zimeanzisha Umoja wa Walimu na Wazazi (Uwawa).

Mwenyekiti wa kamati ya Shule ya Msingi Pambogo ya jijini Mbeya, Gabriel Mbwile amesema muitikio wa wazazi katika vikao na mikutano inayoitishwa shuleni huwa ni ndogo kulinganisha na idadi ya wanafunzi waliopo.

“Utakuta wanakuja wazazi 200 kati ya wanafunzi 1,000 mwisho inapoazimiwa kuchangia mambo ya maendeleo wanalalamika kutoshirikishwa wakati wameitwa kikaoni hawafiki,” amesema Mbwile.

Mbwile amesema wamebuni mbinu za kuanzisha kamati za wazazi kwa madarasa na wawakilishi wake watakuwa na majukumu sawa na kamati za shule.

“Tumegundua wazazi hawaoni umuhimu wa vikao tuliamua kuwanyang’anya mabegi wanafunzi ili kuona mzazi atafanyaje lakini hawakushtuka hivyo tunaamini kamati za madarasa zitasaidia,” amesema.

Habari hii imeandikwa na Devotha Kihwelo(Dar), Saddam Sadick(Mbeya), Janeth Joseph(Moshi) na (Mwanza).

Related Posts