Mwaka 2024 umekuwa wa majonzi kwa taifa kutokana na kuondokewa kwa viongozi wawili mashuhuri wa kitaifa waliopendwa na Watanzania na kufanya makubwa kwa ajili ya nchi yao walipokuwa na dhamana ya uongozi.
Viongozi hawa ni Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambao wote walifariki Februari mwaka huu na kuufanya mwezi huo kuwa wa maombolezo ya kitaifa.
Licha ya kwamba wametangulia, wanakumbukwa kwa kazi kubwa walizozifanya wakati wa uongozi wao, jambo ambalo limewajengea heshima kubwa kwa Watanzania na kukumbukwa kwa mchango walioutoa kwa Taifa.
Viongozi wengi wamefariki dunia mwaka huu, hata hivyo misiba ya viongozi hawa ilikuwa ya tofauti kutokana na mafunzo waliyoyatoa kwa wananchi na viongozi wengine wa sasa, hasa uvumilivu na kujitoa katika kuwatumikia wananchi.
Kati ya viongozi hawa, Lowassa alikuwa wa kwanza kufariki dunia, Februari 10, 2024 saa 8 mchana katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya jijini Dar es Salaam, taarifa iliyowastua Watanzania wengi.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, aliyetangaza kifo hicho, Lowassa, aliyekuwa na umri wa miaka 70, alikuwa akipatiwa matibabu ya magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.
Moja ya mambo ambayo Watanzania wanayakumbuka kwa Lowassa ni kufanya uamuzi mgumu katika mambo ambayo hayakuzoeleka huko nyuma.
Alijenga utamaduni wa uwajibikaji serikalini na watu wasiowajibika waliwajibishwa.
Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu kati ya mwaka 2005 – 2006, alijipambanua kama msimamizi kwelikweli wa shughuli za kila siku za Serikali.
Alitembelea miradi ya maendeleo na akibaini uzembe au ukiukwaji wa taratibu, alichukua hatua papo hapo za kuwawajibisha wahusika.
Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ulioasisiwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ulisimamiwa na Lowassa na alitumia uwezo wake wote kuhakikisha kwamba maono ya Rais yanatekelezwa.
Aliiagiza Mifuko ya Hifadhi za Jamii kushiriki katika ujenzi wa chuo hicho kikubwa barani Afrika.
Mvuto wa Lowassa ulidhihirika zaidi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambapo aligombea urais ndani ya CCM lakini jina lake lilikatwa, jambo lililowakera wajumbe wa mkutano mkuu huo ambao walisikika wakiimba “tuna imani na Lowassa.”
Safari yake haikuishia hapo, alianzisha safari nyingine “ya matumaini” kwa kujiunga na Chadema na kupata nafasi ya kugombea urais ambapo aliendelea kupata umaarufu zaidi katika kampeni zake zilizojaza maelfu ya Watanzania.
Aliweka rekodi ya kuwa mgombea wa kwanza wa upinzani aliyepata kura nyingi za urais.
Lowassa alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote dhidi ya John Magufuli wa CCM aliyeshinda kwa kupata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46.
Lowassa aliwezesha pia Chadema kupata idadi kubwa ya wabunge ambayo haikuwahi kufikiwa na upinzani.
Hata hivyo, Machi Mosi, 2019, Lowassa alirejea CCM na kupokelewa na Rais Magufuli, tangu wakati huo alikuwa akipatiwa matibabu hadi alipofariki.
Mwinyi, aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, alifariki dunia Alhamisi Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu. Alifariki akiwa na umri wa miaka 98.
Kiongozi huyo mstaafu, anakumbukwa kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa aliyoyafanya Zanzibar na Tanzania Bara, hasa kutokana na kwamba alipokea kijiti cha uongozi katika kipindi ambacho nchi ilikuwa na hali mbaya.
Alianza kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa kuruhusu wawekezaji kuja nchini na Watanzania pia kuagiza bidhaa kutoka nje na pia kwenda kuuza nje, jambo ambalo huko nyuma lilitazamwa kama ulanguzi.
Kutokana na uamuzi wake huo, nchi ilifunguka, bidhaa nyingi ziliingia nchini, vituo vya televisheni vya binafsi vilianzishwa, maisha ya wananchi yaliboreka na uchumi wa Tanzania ulianza kukua.
Taasisi za fedha za kimataifa zilianza kuikopesha Tanzania.
Kauli yake ya ‘ruksa’ ilikuwa na matokeo makubwa kwenye maisha ya Watanzania.
Yeye ndiye kiongozi aliyezalisha mabilionea waliopo sasa, akiwamo Bakhresa ambao walitumia fursa na mazingira wezeshi aliyoyajenga kujiinua kibiashara na kiuwekezaji.
Mbali na mageuzi ya kiuchumi, Mwinyi alifanya mageuzi ya kisiasa kwa kuruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na hatimaye mwaka 1995, Tanzania ikafanya uchaguzi wake wa kwanza uliohusisha vyama vingi.
Aliondoka madarakani mwaka 1995 akiwa ameiacha nchi ikiwa na msingi mzuri kwa viongozi waliomfuatia kuendelea kuijenga.
Rais Benjamin Mkapa, aliyemfuatia aliendeleza mageuzi hayo kwa kupigania utandawazi uliochochewa na dhana ya ruksa.
Sifa nyingine aliyokuwa nayo Mzee Mwinyi ni uadilifu, ukarimu na ucheshi wake hasa kupitia misemo yake ya Kiswahili fasaha yenye mafunzo ndani yake na iliyokuwa ikifikisha na kukumbusha kuhusu umuhimu wa kutenda mema.
Wachambuzi wa siasa nchini wanaeleza mambo ya kujifunza kutokana na maisha ya Lowassa na Mwinyi ambapo kila mmoja amebeba sura ya kipekee katika uongozi, ikiwemo uchapakazi, uadilifu na uongozi wa kuwatumikia wananchi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema kila mmoja alikuwa na karama zake za pekee ambazo ni mafunzo kwa viongozi wa sasa, hasa vijana waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi.
“Ukimwangalia Lowassa, ni aina ya kiongozi anayependa kuona matokeo, anapenda mkijadili jambo basi litekelezwe. Kwenye hilo alifanikiwa sana na wananchi walipenda mtindo wake wa uongozi hasa katika kusimamia utekelezaji wa miradi,” anasema.
Kwa upande wa Mzee Mwinyi, Dk Loisulie anasema anatoa somo la uadilifu wa kiwango cha juu kwa kuwa hakuwa na makuu, hakujilimbikizia mali na pia hana visasi kwa wabaya wake, jambo ambalo lipo kwa viongozi wachache.
Akiwa na mtazamo kama huo, mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza anasema kila mmoja alifanya kazi kwa kadiri ya uwezo wake na mazingira yaliyokuwepo wakati huo, hivyo wanatoa somo la kukabiliana na mazingira uliyonayo.
“Kila mmoja alikuwa na upekee wake na ndiyo sifa ya kiongozi. Mwinyi alikuwa mwadilifu na kiongozi mtulivu, aliliongoza taifa katika mabadiliko makubwa miaka ya 1990,” anasema mchambuzi huyo wa siasa.