Mama mbaroni tuhuma ya kumfukia shimoni kichanga cha siku moja

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia Subira John (25), mkazi wa Mtendeni, Kilosa kwa tuhuma za kumfukia shimoni mtoto wake na kumtelekeza muda mfupi baada ya kumzaa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema binti huyo amekamatwa baada ya uchunguzi wa kina tangu tukio hilo litokee Desemba 2, 2024.

“Mtuhumiwa alikamatwa akiwa amejificha kwenye nyumba ya wageni isiyo rasmi maarufu ‘gesti bubu’ huko Kilosa,”amesema Kamanda Mkama.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, binti huyo alifanya tukio hilo Novemba 8, 2024 katika eneo la K Park Bar, Kitongoji cha Mbumi, Kata ya Mbumi na mtuhumiwa anadaiwa kumfukia mtoto wake huyo mchanga wa siku moja mwenye jinsia ya kiume kwenye shimo na kisha kumtelekeza.

Taarifa imeeleza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na idara ya ustawi wa jamii walifanikiwa kumchukua mtoto huyo na kumpeleka kituo cha kulelea watoto cha Mgolole kilichopo Manispaa ya Morogoro. Kwa sasa hali ya mtoto inaendelea vizuri.

“Upelelezi wa tukio hilo unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa utakapokamilika,”imeeleza taarifa hiyo.

(Imeandikwa na Happiness Mremi)

Related Posts