Mambo bado kesi ya ‘Dk Manguruwe’

Dar es Salaam. Serikali inaendelea na upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu Dk Manguruwe na mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, Rweyemamu John (59).

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 28, yakiweno ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha, kinyume cha sheria.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameeleza hayo leo Jumatano, Desemba 4, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesi ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Kasala amedai upelelezi unaendelea, hivyo kuomba Mahakama ipange tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo, mshtakiwa wa pili, Rweyemamu aliiomba Mahakama impatie masharti ya dhamana kwa kuwa hana shtaka la kutakatisha fedha.

Hakimu Magutu ametoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa Rweyemamu akimtaka awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka Serikali ya mtaa au taasisi inayotambulika kisheria.

Pia mshtakiwa anatakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh45 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.Hakimu Magutu amesema iwapo mshtakiwa atatimiza masharti, atakuwa nje kwa dhamana.

Mshtakiwa Mkondya hana dhamana kutokana na shtaka la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Hakimu ameahirisha kesi hadi Desemba 18, 2024 itakapotajwa. Kesi imesikilizwa kwa njia ya video, washtakiwa wakiwa rumande.

Katika kesi ya msingi, kati ya mashtaka hayo 28, mashtaka 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka tisa ni ya kutakatisha viwanja.

Wanadaiwa kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba mosi, 2023 jijini Dar es Salaam, walitenda makosa ya kuendesha upatu kinyume cha sheria.

Inadaiwa Mkondya akiwa mkurugenzi wa kampuni na John mkaguzi, waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata fedha mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya walizotoa.

Wanadaiwa kujipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 waliotoa kiasi tofauti cha fedha kwa ahadi watapata faida mara mbili hadi tatu ya kiasi walichotoa.

Katika mashtaka tisa ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee, anadaiwa kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba mosi, 2023, mkoani Dar es Salaam akiwa mkurugenzi wa kampuni alijipatia viwanja tisa vilivyopo kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Anadaiwa kujipatia viwanja hivyo akijua ni zao la makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.

Related Posts