MBUNGE wa Jimbo la Segerea Bonnah Kamoli, amesema yuko tayari kutoa fedha zake kugharamia uondoaji mawe makubwa yaliyotumika na mfanyabiashara mmoja anayemiliki kituo cha mafuta kufunga njia na kusababisha adha kubwa kwa wananchi kando ya daraja la juu linalovuka Reli ya SGR, Uwanja wa Ndege, Kata ya Kipawa, jijini Dar es Salaam.
Aidha mfanyabiashara huyo ametakiwa kujenga sehemu aliyoboa ya daraja hilo alipokuwa akiweka mawe hayo.
Bonnah ambaye leo alifika katika eneo hilo, amesema mfanyabiashara huyo alipewa siku 14 aondoe mawe hayo na na kujenga sehemu ya daraja aliyobomoa lakini hajatekeleza.
“Mimi nimeamua nitatoa fedha zangu, kesho Mwenyekiti wa CCM Kata, Diwani na uongozi wa kata wasimamie uondoaji wa mawe haya. Yasogezwe yawekwe pembeni wananchi watumie njia hii,”amesema Bonnah.
Wananchi wa eneo hilo, walimshukuru Mbunge huyo kwa uamuzi huyo kwani hatua ya mfanyabiashara huyo kuziba njia katika eneo ambalo siyo mali yake kiliwapa adha kubwa kupia kwenda katika nyumba zao na kufanya shughuli zingine muhimu.
Katika hatua nyingine, Bonnah ametembelea Soko la Buguruni kusikiliza kero za wananchi hususan sehemu ya kuchinjia kuku na kuahidi kuifanyia kazi.
Changamoto nyingine ni ya wafanyabiashara kuomba Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kurejesha choo cha umma katika soko hilo katika uongozi wa soko badala ya kuendeshwa na halmashauri hiyo.
Bonnah aliahidi kuzitafutia ufumbuzi kero hizo haraka iwezekanavyo hivyo kuwataka wafanyabiashara kuendelea kutekeleza majukumu yao.