Namibia yamchagua rais wa kwanza mwanamke

Windhoek, Namibia

Netumbo Nandi-Ndaitwah, kutoka Chama tawala cha South West Africa People’s Organisation (Swapo), amepigiwa kura kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Namibia baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita.

Tume ya uchaguzi ilisema ameshinda zaidi ya 57% ya kura, huku mpinzani wake wa karibu Panduleni Itula akipata 26%.

Kufuatia matatizo ya vifaa na kuongezwa kwa siku tatu kwa upigaji kura katika baadhi ya maeneo ya nchi, Itula alisema mchakato wa uchaguzi “una dosari kubwa.”

Chama chake cha Independent Patriots for Change (IPC) kimesema kinapinga matokeo hayo mahakamani.

Vyama vingi vya upinzani vilisusia matokeo yaliyotagazwa Jumanne jioni katika mji mkuu, Windhoek, gazeti la Namibia linaripoti.

Swapo imekuwa madarakani katika nchi hiyo kubwa lakini yenye wakazi wachache kusini mwa Afrika tangu uhuru mwaka 1990.

Nandi-Ndaitwah, ambaye kwa sasa ni makamu wa rais, amehudumu katika nafasi kubwa za serikali kwa robo karne.

Related Posts