Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Taifa, Othman Masoud, amesema ni wajibu kwa wananchi wa Zanzibar kuonyesha mshikamano katika kupigania haki zao za msingi, zikiwemo za utambulisho na masilahi ya nchi yao.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema hayo alipozungumza na wananchi wa Shehia ya Mjananza Wingwi, Jimbo la Pandani, Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Wajibu huo unakuja kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali wasiofuata maadili, miongozo na misingi ya uongozi, bali huendekeza vilemba vya kisiasa kwa kuwagawa wananchi na hata kukandamiza haki zao,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kitengo cha habari Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, leo Jumatano, Desemba 4, 2024, Othman amesema yapo mambo mengi ya msingi yameainishwa katika Katiba ya Zanzibar, lakini wapo baadhi ya viongozi wanaoyapindisha kwa kuendekeza masilahi binafsi.
“Hatuna budi kuungana pamoja kwa kuyakataa hayo, na kisha kuiweka madarakani ACT- Wazalendo, kwa ajili ya kuja kulinda heshima, utu, thamani ya kila mtu na kuilinda Katiba ya Zanzibar,” amesema.
Amewataka wananchi kukiwajibisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kukiondoa madarakani kupitia sanduku la kura wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025.
“Mwenendo wa baadhi ya viongozi hasa wa ngazi ya sheha, wilaya na mikoa, ambao kisheria ni watumishi wa umma, lakini hujivisha zaidi wajibu na itikadi za vyama vya siasa jambo ambalo halikubaliki, hivyo ni wakati sasa kutafuta mbadala kurejesha nidhamu katika kuongoza nchi,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo -Zanzibar, Omar Ali Shehe, amesisitiza haja ya wananchi kujitokeza kwa wingi katika awamu ya mwisho ya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura linalotarajiwa kuanza Februari 2025, kama hatua muhimu ya kupigania heshima na mageuzi ya kweli ya kuiongoza Zanzibar.
Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kichama wa Wete, Juma Khamis Ali, amesema mwelekeo wao kwa sasa ni kuhamasisha uungwaji mkono mkubwa wa wananchi, ili kupata viongozi bora, wenye nidhamu na maadili, kuanzia ngazi za chini.