Sh2.8 bilioni za mradi wa maji kunufaisha vijiji 16 Katavi

Katavi. Wakazi zaidi ya 64,000 kutoka vijiji 16 wilayani Mlele Mkoa wa Katavi, wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji wa Bwawa la Nsekwa wenye thamani ya Sh2.8 bilioni.

Akitoa taarifa hiyo leo Jumatano, Desemba 4, 2024 mbele ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi, iliyotembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Charles Mengo amesema mradi umesanifiwa kwa lengo la kusambaza maji safi na salama kwa wananchi wa Mlele, huku ukilenga kuondoa adha kwa wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Mengo amevitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na cha Inyonga na Kalampaka vilivyopo Kata ya Inyonga; Utege, Ngome na Achauseme katika Kata ya Utende; Mtakuja, Nsekwa na Kalolo katika Kata ya Nsekwa; Ipwaga, Mapili na Masigo vilivyopo Kata ya Ileja pamoja na Kamsisi, Malabuki, na Songambele vilivyopo Kata ya Kamsisi.

Kwa mujibu wa Mengo, bwawa hilo lilisanifiwa mwaka 2016 na lina uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 2 za maji.

Amesema ujenzi wake mpaka sasa umefikia asilimia 90 na kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa tuta la kuzuia maji, kuweka mawe, ujenzi wa chemba ya kutolea maji, ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo, ujenzi wa daraja dogo na ujenzi wa nyumba ya usimamizi wa mradi.

Amesisitiza kuwa hatua hizo zimefikia kiwango cha juu na mradi upo hatua za mwisho za utekelezaji wake.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta ametoa rai kwa Ruwasa kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, ili wananchi waanze kunufaika.

“Tumetembelea Bwawa la Nsekwa na kuona hatua iliyofikiwa. Kazi inaendelea vizuri, lakini tunatoa wito kwa Ruwasa kuhakikisha wakandarasi wanasimamia vema mradi huu ili ukamilike haraka,” amesema Kimanta.

Amesema lengo la Serikali ni kuona huduma ya maji inafikia asilimia 85 vijijini na asilimia 90 mijini ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoelekezwa kwenye ilani ya chama hicho.

Lusia Enock mkazi wa kijiji cha Ipwaga amesema mradi huo utawapunguzia changamoto ya maji, hasa kipindi cha kiangazi.

“Tunateseka sana kutafuta maji hasa wakati wa kiangazi, tunatembea umbali wa kilometa tano hadi sita. Mradi huu ukikamilika, tutapata maji karibu na makazi yetu na kuondokana na changamoto hizo,” amesema.

Amesema hata kero walizokuwa wanakumbana nazo nyumbani zitapungua, kwani wamekuwa wakichelewa kurudi nyumbani kutokana na kutafuta maji hali iliyokuwa ikisababisha migogoro na waume zao.

Related Posts