Taasisi ya GSM Foundation yaendelea kuchangia jitihada za serikali katika uhifadhi wa taka kwa Shule za Msingi.

Katika jitihada zake za kuimarisha utunzaji wa mazingira na kukuza elimu ya uhifadhi wa taka kwa wanafunzi wa shule za msingi, Taasisi ya GSM Foundation imetoa msaada wa vifaa vya kuhifadhia taka kwa Shule ya Msingi Jangwani Beach, Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na usimikaji wa mapipa 12 ya kuhifadhia taka kwa matumizi ya nje ya madarasa, vipipa taka 25 vya ndani ya madarasa, toroli moja la usafirishaji wa taka na kubandika mabango 50 yenye jumbe za kimazingira kwenye mazingira ya shule.

Mpango huu ni sehemu ya dhamira ya GSM Foundation ya kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kimkakati wa Hifadhi ya Mazingira wa mwaka 2022-2032, (NATIONAL ENVIRONMENTAL MASTER PLAN FOR STRATEGIC INTERVENTIONS 2022–2032) unaolenga kuboresha usimamizi wa taka na mazingira nchini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mkuu wa taasisi ya GSM Foundation, Bi. Faith Gugu alisema:


“Mkakati wetu ni zaidi ya utoaji wa vifaa vya kuhifadhi taka. Tunakusudia kukuza uwajibikaji wa kimazingira kwa watoto wetu kwa kuwapa elimu ya mbinu bora za usimamizi wa taka. Lengo ni kuwawezesha wanafunzi hawa kuwa mabalozi wa mazingira safi katika familia na jamii zao, hivyo kuleta mabadiliko ya kudumu na kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.”

Mbali na msaada huu kwa Shule ya Msingi Jangwani Beach, GSM Foundation tayari imetoa vifaa vingine na kuhamasisha elimu ya mazingira kwa shule za msingi tatu katika Wilaya ya Kinondoni. Jitihada izo zilihusisha utoaji na usimikijai wa mapipa taka 55, vidumutaka 65 vya ndani ya madarasa, na matoroli matano, ambavyo vimewanufaisha wanafunzi wapatao zaidi ya 5,000 na walimu zaidi ya 200.

Pia, jumla ya mabango 200 yenye ujumbe wa elimu ya mazingira yamewekwa katika maeneo tofauti mashuleni, huku Shule ya Msingi Jangwani Beach ikipokea mabango 50. Mabango haya yanasaidia kuhamasisha uwajibikaji wa mazingira miongoni mwa wanafunzi na jamii zinazozunguka shule hizo.

Aidha, mpango huu unalenga pia kuleta manufaa ya kiuchumi kwa jamii kupitia uhifadhi sahihi wa taka, ambapo taka zinazoweza kuchakatwa zitakuwa chanzo cha kipato kwa familia zilizo karibu na shule.

“Tunaamini kuwa kila hatua ni muhimu,” alisema Bwana. Rajabu Kondo, Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya GSM. “Kwa kushirikiana, tunaweza kuleta mabadiliko ya kudumu katika usimamizi wa mazingira na kujenga jamii endelevu.”

GSM Foundation imepanga kuendeleza juhudi hizi kwa kutoa msaada wa vifaa vya kuhifadhi taka kwa shule moja kila mwezi hadi Juni 2025.


Related Posts