TARI Tengeru yatambulisha Mbegu mpya aina 19 za mbogamboga

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha TARI Tengeru iko hatua za mwisho za usajili wa Mbegu mpya bora aina 19 za mbogamboga zinazolenga kuongeza tija katika mnyororo mzima thamani wa Kilimo cha mbogamboga.

Mbegu hizo zinatajwa kuwa na sifa za kuhimili magonjwa, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na zina mavuno mengi.

Hayo yameelezwa leo Desemba 04, 2024 Jijini Dar es Salaam na Watafiti wa TARI Katika Mafunzo kwa wadau wa mnyororo wa thamani wa mbogamboga yanayolenga kujenga uelewa na uhamasisha wa ujio wa Mbegu hizo za pilipili kichaa (5), pilipili hoho (5), Pilipili Mbuzi(3), na nyanya(6).

Emanuel Lasway- Mtafiti mwandamizi kituo cha TARI Tengeru na mratibu kitaifa wa Utafiti wa mbogamboga anasema wamefanya majaribio ya Mbegu hizo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na Iringa ambapo zimefanya vizuri.

Zaidi, Lasway- amesema ujio wa Mbegu hizo unalenga kumpunguzia Mkulima gharama za uzalishaji kutokana kuwa ni stamilivu za magonjwa hivyo kupunguza matumizi ya viuatilifu.

Naye Mkurugenzi idara ya Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano wa TARI Dkt Sophia Kashenge amesema ujio wa Mbegu hizo ambazo ni za uchavushaji huru (OPV) ni Moja ya matokeo ya kazi mbalimbali nzuri na muhimu zinazofanywa na watafiti wa TARI kuhakikisha wanaleta Teknolojia zinazojibu changamoto hasi za mabadiliko ya tabianchi ambayo hupunguza tija katika Kilimo.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Jiji la Dar es Salaam Bi.Tabu Shaibu ameipongeza TARI kwa kufanya tafiti mbalimbali zinazochangia usalama na utoshelevu wa chakula nchini.

Bi Tabu amekiri kujifunza mengi kuhusu kilimo kupitia kikao hiki na hivyo kutumia nafasi hiyo kuwaasa wadau wa Kilimo nchini kupata taarifa sahihi kwa Watafiti ili kubadili maisha yao kutokana na tija inayopatikana katika Kilimo.

Kwa upande wake,mshikiri wa kikao hicho, Bw. Sebastian Kombe ambaye ni Msambazaji wa Pembejeo za Kilimo amesema ujio wa Mbegu hizo ni tija kutokana zinamsaidia uhakika wa upatikanaji wa Mbegu bora zitakazomsaidia kuwa na soko la uhakika kwa Wakulima.

Related Posts