NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imeipongeza Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania kwa kufadhili na kugharamia programu ya kuendeleza ujuzi yaani ‘‘Skills for their Future’’ ya kuwajengea walimu pamoja na wanafunzi uwezo wa kutumia TEHAMA katika Shughuli zao mbalimbali ikiwemo shughuli za kitaaluma pamoja na bunifu mbalimbali kwa kushirikiana na Mfuko wa Elimu wa Taifa.
BRAC – Maendeleo Tanzania kwa kushirikiana na TEA imetekeleza program hiyo katika shule za sekondari za Karibuni, Miburani na Wailes zilizopo halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam ambapo ulianza mwaka mwaka 2022.
Akizungumza leo Disemba 4, 2024 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kufunga Mradi wa ‘‘skills for their future’’ unaotoa mafunzo ya kidigitali kwa vijana katika shule hizo, Kaimu Meneja Usimamizi Miradi ya Elimu wa TEA, Bi. Mwafatma Mohamedi amesema Program hii ni ya kipekee katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na TEA wanaona fahari kushirikiana na taasisi hiyo katika juhudi za kuboresha elimu na maendeleo ya taifa letu.
Amesema mwaka 2022 Februari 10, TEA ilisaini makubaliano maalum ya Ushirikiano na Shirika la BRAC – Maendeleo Tanzania ambalo ni mdau muhimu wa maendeleo katika Sekta ya Elimu nchini.
Aidha amesema, TEA inajivunia kusaini makubaliano hayo kwani yanachangia kusukuma mbele jitihada za nchi katika kufikia lengo namba nne la Maendeleo Endelevu ya Millenia linalohimiza elimu bora, yenye usawa na kutoa fursa kwa wote kujiendeleza.
Amesema Kupitia makubaliano hayo, BRAC – Maendeleo Tanzania, ilitoa jumla ya Kompyuta 120 ambazo zinajumuisha Kompyuta Mpakato 60 na Tablet 60, zikiwa na thamani ya Shilingi Milioni 132.6.
“Kompyuta hizo zilipelekwa katika shule tatu (3) za Sekondari katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ambazo ni Miburani, Wailes na Karibuni lengo likiwa ni kunufaisha wanafunzi 600 na walimu 26 wa shule hizo”. Amesema Bi. Mwafatma.
Amesema shule hizo zilinufaika na ukarabati wa vyumba maalum vya kompyuta (Computer Lab) ili kutoa fursa kwa wanafunzi na walimu kujifunza kwa vitendo elimu ya Kompyuta (TEHAMA).
Kwa upande wa mwakilishi wa Mkurugenzi wa BRAC – Maendeleo Tanzania, Bi. Kalunde Simba amesema Changamoto ya wanawake na wasichana wanaojihusisha na TEHAMA inachangiwa na ukosefu wa miundombinu ya kutosha na pia ujuzi mdogo wa walimu kuweza kutoa mafunzo husika kwa wanafunzi.
Sanjari na hayo amesema vikwazo vya kijamii na kitamaduni ambapo wazazi wanapendelea wavulana zaidi ya wasichana, hasa katika elimu, imesababisha wasichana wachache kupata mafunzo ya teknolojia, kuwa na ujuzi unaohitajika wa kufanya kazi za teknolojia na hivyo kuwatenga wasichana nje ya njia muhimu za kazi katika sekta ya teknolojia.
Vilevile amesema ushirikiano huo umechangia Kuboresha uwezo wa walimu wasiopungua 64 katika shule 3 za sekondari ambazo ni Shule za Karibuni, Miburani na Wailes zilizopo wilaya ya Temeke – Dar es Salaam, kutoa mafunzo bora ya kusoma na kuandika kwa njia ya kidigitali.
Nae Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Temeke, Bi. Niconia Amos amewapongeza BRAC Maendeleo Tanzania kwa kutekeleza na kufanikisha mradi wa “Skills for Their Future” katika shule hizo kwani Mradi huo umekuwa chachu ya maendeleo kwa wanafunzi, hususan wasichana balehe na wanawake vijana
Ameeleza kuwa wanafunzi 1,922 na walimu 64 wamepata mafunzo ya maarifa ya kidigitali na vifaa vya TEHAMA vilivyotolewa vimeongeza uwezo wa shule zetu katika kutoa elimu bora kwa vitendo.