Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ametoa maoni kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliopita, akibainisha kasoro zilizojitokeza na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua.
Jaji Warioba aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania ametaka Chama cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani kuweka masilahi yao pembeni na kujadili changamoto zilizojitokeza.
Ametoa kauli hiyo leo Desemba 4, 2024 wakati matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Novemba 27, 2024 yakitoa ushindi kwa CCM kwa asilimia 99, huku vyama vya upinzani vikiulalamikia baadhi vikitaka matokeo yafutwe.
Miongoni mwa malalamiko kuhusu uchaguzi huo ni wagombea wa upinzani kuenguliwa na baadhi ya makada wa vyama hivyo na wa CCM kudaiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jaji Warioba amezungumzia uchaguzi huo, akigusia na wa mwaka 2025 akieleza anachokiona mbele iwapo hatua hazitachukuliwa.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, licha ya changamoto hizo zilizoibuka katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019, bado zimejirudia akionya zisiposhughulikiwa ipasavyo zinaweza kuleta machafuko ya kisiasa kama yaliyotokea mwaka 2000 Zanzibar.
“Nimeona Serikali imesema uchaguzi umefanikiwa kwa asilimia 100, unawezaje kusema hivi wakati watu wanakufa? Ilinishtua,” amesema.
“Nimesikiliza maelezo ya Serikali lakini hayakutosha, haiwezekani kwamba wananchi waamini walioenguliwa, walikosea tena kwa maelfu, lakini wanaoenguliwa ni upande mmoja. Kuna vyama ambavyo wanachama wake wanajua kufuata masharti na kuna vyama havijui.
“Haiwezekani na wala tusijedanganyika kuwa kuna maelezo kwamba sababu kubwa hawakufuata masharti, tutakuwa tumejidanganya kama tutakuwa tumeamini, haiwezekani kunatokea kura bandia, zilizotokea mwaka 2020, zikatokea mwaka huu, zamani zilikuwa zinaandaliwa na wagombea, kura bandia za sasa ukiangalia zimeandaliwa na wasimamizi wa uchaguzi,” amedai Jaji Warioba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jaji Warioba amesema matatizo ya uchaguzi wa mwaka 2000 yaliyotokea Zanzibar na kusababisha maandamano, vurugu kubwa, kusababisha vifo na majeruhi, anaona hayo yakijirudia.
“Ilikuwa hali ngumu kushawishi CUF na CCM kufanya mazungumzo na kuwa kitu kimoja. Tusipopata njia ya kumaliza matatizo hayo tutafikia hali ya kama Zanzibar ya mwaka 2000,” amesema.
“Tuna wasiwasi mkubwa haya matatizo siyo ya CCM bali Serikali ambayo imejitenga na CCM, si mmeona matamko ya katibu mkuu? Msimamo wa CCM siyo kama ambavyo wamefanya wasimamizi wa uchaguzi.
“Amani imepungua sana, tusifikirie amani ni utulivu tu, lakini kuna watu wana hofu na maisha yao,” amesema.
Vurugu za uchaguzi wa Zanzibar ziliibuka Januari 27, 2001 zilitokana na maandamano yaliyoandaliwa na CUF wakipinga matokeo ya uchaguzi mkuu na yalifanyika katika Jiji la Dar es Salaam, Unguja na Pemba.
Katika maandamano hayo, baadhi ya watu walifariki dunia huku wengine wakijeruhiwa na wengine wakikimbilia nchini Kenya.
Hata hivyo, Novemba 16 Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alipozungumzia rufaa zilizokatwa na wagombea, 16,309 zilipokewa na kati ya hizo rufaa 5,589 zilikubaliwa.
Alipozungumzia kuhusu mwenendo wa uchaguzi usiku wa Novemba 27, Mchengerwa alisema kwa asilimia 98 ulikwenda vizuri na hata malalamiko hayakuwa mengi na kwamba, yanapotokea yanasaidia kusonga mbele kwa ajili ya kujipanga na chaguzi zijazo.
Baada ya maoni ya Jaji Warioba, Mwananchi limemtafuta Waziri Mchengerwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Adolf Ndunguru lakini hawakupatikana simu zao ziliita pasipo kupokewa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi alipotafutwa alishauri atafutwe Mchengerwa.
“Nipo kwenye kikao… muulize Waziri wa Tamisemi,” amesema Lukuvi.
Rais Samia akizungumzia uchaguzi huo Novemba 26, aliwataka wasimamizi wa uchaguzi na wanaohusika, kuhakikisha unakuwa wa haki, uwazi kwa kuzingatia taratibu zilizokubaliwa na wadau.
“Napenda kuwahakikishia kuwa uamuzi wenu katika sanduku la kura utaheshimiwa,” alisema.
Mbali ya hayo, Jaji Warioba ameonya vyombo vya ulinzi kuhusishwa na siasa, akidai kwa sasa Jeshi la Polisi limeingizwa kwenye siasa.
“Katika miaka michache iliyopita tumeliingiza Jeshi la Polisi kwenye siasa, linatoa matamko ya kisiasa na hii italeta mgawanyiko. Wananchi watagawanyika. Kuna wale watakaoona, Jeshi la Polisi ni adui, tusifike huko. Tuliache Jeshi la Polisi lifanye kazi zake za kawaida,” amesema.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alipotafutwa kuhusu madai hayo ya Jaji Warioba hakutoa majibu.
“Uchaguzi umekuwa kama hali ya hatari na vyombo vya ulinzi vinaandaliwa,” amedai akitoa mfano wa hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia mkutano wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) na kusababisha viongozi wakuu wa chama hicho kukamatwa jijini Mbeya Agosti 12, 2024 akisema yalikuwa ni mambo ya siasa.
“Si mnafahamu kilichotokea Mbeya Katibu Mkuu (CCM- Dk Emmanuel Nchimbi), alisema hayo mambo ya siasa waachiwe huru, sasa ile siyo njia nzuri tutafute njia sahihi,” amesema.
Amesema kwa bahati nzuri Rais (Samia Suluhu Hassan) alipoingia madarakani alisikia malalamiko ya wananchi kuhusu suala hilo na aliunda Tume ya Haki Jinai.
“Tume ikaleta mapendekezo mazuri na ikapendekeza, Jeshi la Polisi liachwe lifanye kazi zake, lakini sasa hivi tumeliingiza Jeshi la Polisi kwenye siasa. Chombo kikubwa kama polisi kugawanyika kuna hatari,” amedai.
Akijibu swali la Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahiriri Tanzania (TEF), Deodatus Balile kuhusu uwezo wa vyama vya upinzani kuweka wagombea maeneo mengi ili visishindwe kabla ya kuingia kwenye mchakato Jaji Warioba alisema:
“Mimi nazungumza na watu wengi sina mipaka, nazungumza na viongozi wa vyama vyote, si muda mrefu imepita kama miezi sita hivi nilimuuliza kiongozi mmoja wa upinzani je, wanategemea nini, akaniambia walifanya utafiti kuona hali itakavyokuwa.
“Matokeo yake akaniambia wakijitahidi sana upinzani wote katika uchaguzi wowote unaokuja hawazidi asilimia 25, wakijua kwamba wao kwa wakati huo hawana uwezo wa kutoa ushindani. Nikauliza kwa nini? Akanijibu miaka sita shughuli za kisiasa ziliwakwamisha hawakufanya kazi, sasa ndiyo wanaanza hawajasambaa kwenda chini.”
“Kwa hiyo ukija uchaguzi kuna mahali hawataweza kuweka wagombea, walisema watapata asilimia 25 kwa sababu hawana uwezo wa kuweka wagombea, lakini hata walipokuwa na uwezo wa kuweka wagombea wameenguliwa,” amesema Jaji Warioba.
Malalamiko ya 2019 yamejirudia
Jaji Warioba amesema licha ya malalamiko ya uchaguzi kuwepo tangu mwaka 2019 bado yameendelea kujirudia, akionya hali itakuwa mbaya kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.
“Tumeona mjadala huu tangu 2019, imani iliyokuwepo kwamba uchaguzi wa mwaka huu hautafanana na ule wa 2019, lakini matokeo yake ni vilevile. Uchaguzi wa mwaka kesho kama tusipochukua hatua utakuwa kama huu,” amesema.
“Tume itakayosimamia uchaguzi wa mwaka kesho ni ileile iliyosimamia uchaguzi wa 2020, maana sioni dalili pamoja na sheria kupitishwa,” amesema.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima alipozungumza Juni 13, 2024 kwenye mkutano wa tume na wanahabari kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura alisema hakuna kifungu chochote cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kinachowalazimisha wajumbe wa tume hiyo kujiuzulu na kupisha wengine.
Alisema uhalali wa nafasi za wajumbe unatokana na kifungu cha 27 cha Sheria ya INEC ya mwaka 2024.
Jaji Warioba amesema chanzo cha changamoto za uchaguzi kujirudia ni kukwama kwa utawala bora katika utawala wa Hayati Rais John Magufuli ulioingia madarakani Novemba 2015 hadi Machi 17, 2021 alipofariki dunia akiwa madarakani.
“Rais Magufuli aliacha kumbukumbu kubwa na atakumbukwa kwa muda mrefu katika eneo la kuendeleza miundombinu,” amesema akitaja uamuzi aliosimamia wa Serikali kuhamia Dodoma, ujenzi wa miundombinu kama barabara, madaraja, reli ya kisasa na Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).
“Kwa kuendeleza vitu Magufuli ameacha kumbukumbu, lakini kwa utawala bora, hakufanya vizuri. Kwanza alisema Katiba siyo kipaumbele na haya yote aliyofanya kwa kiwango kikubwa yalikuwa kinyume cha Katiba,” amesema.
Amesema Rais Samia aliyeingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya kifo cha Dk Magufuli amekuwa akiendeleza mambo mazuri aliyoacha mtangulizi wake na kurekebisha yaliyokosewa.
Katika hayo, ameshauri Rais Samia kuchukua hatua kwa malalamiko ya uchaguzi.
Hatua nyingine ni vyama vya upinzani kutokata tamaa bali vijielekeze kwenye mazungumzo na CCM kuwahusisha viongozi wazee kujadili suala hilo kama ambavyo Rais Samia alikuja na falsafa ya 4R (ustahimilivu, kujenga upya, mageuzi na maridhiano).
“Alileta hadi 4R, haikuwa kazi rahisi, lakini aliweza kukubalia ushauri na kuondoa vizuizi vya mikutano ya siasa, maandamano na vyombo vya habari kwa kulegaza masharti ya watu kuwa uhuru ni kazi nzuri aliyoifanya,” amesema.
“Hakuishia hapo aliendelea na mazungumzo hadi kufika mahali, kwamba wataunda chombo kitakachoshauri namna ya kumaliza matatizo ya Kikatiba. Aliona aunde Tume ya Haki Jinai, aliunda tume ya kuangalia sera yetu ya uhusiano wa mambo ya nje,” amesema.
Amesema Rais Samia alikuwa anakwenda vizuri ili Taifa lipate mwafaka, sasa sintofahamu imejitokeza (ya uchaguzi serikali za mitaa) imerudisha nyuma, lakini pamoja na hayo kutokea, anaweza kuingilia kati.
“Alianza na mazungumzo mpaka ikafika mahali wakasema kitaundwa chombo ambacho kitashauri ili tuje tumalize matatizo tuliyonayo. Tukawa tunangojea chombo kile, badala yake ikatakiwa itolewe elimu ya Katiba kwa wananchi. Mpaka sasa sijaona, nadhani ilikuwa ni mbinu ya kuzuia kile alichokiagiza Rais,” amesema.
Kuhusu vyama vya siasa amesema ingawa havina uhusiano mzuri miongoni mwao kwa sababu ya uadui, kukata tamaa, chuki na kutoaminiana, bado vinapaswa kuangalia masilahi ya Taifa.