VETA YABUNI DAWA YA KUKABILIANA NA UTI NA FANGASI

Na Avila Kakingo
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA), imebuni dawa ya kukabiliana na ugonjwa ya maambukizi ya bakteria kwa njia ya mkojo (UTI) na fangasi inayoitwa Lab Spray Disinfectant.
Mwalimu wa Maabara Kutoka VETA Chang’ombe, Ally Issa ameyasema hayo  katika Kongamano na maonyesho ya tisa ya Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu (STICE) linalohitimishwa Desemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam.
Amesema bakteria wengi wa magonjwa hayo hupatikana kwenye vyoo vya umma hivyo, kabla ya kutumia choo unapulizia dawa hiyo kisha unatumia.
“Kama unasumbuliwa na fangasi kwenye miguu unachukua dawa hiyo na kuipulizia kwenye eneo lililoathirika. Dawa hii imetengenezwa na Glycerin, Ethanol, Benzoic na Salicylic kwa ajili ya kuua bakretia wa UTI na fangasi,” ameeleza.
Mwalimu Issa amesema dawa hiyo ina ujazo wa mililita 120 na kuuzwa kwa Sh 4,000 na inapatikana kwenye vyuo vya VETA.

Pia kitengo hicho kimetengeneza mafuta ya mwarobaini kwa ajili ya kujikinga na kudhibiti mbu.

Issa amesema mafuta hayo yametengenezwa kwa utaratibu maalum kwa kutumia majani ya mwarobaini, mchaichai na mafuta ya nazi.
“Mafuta haya hayana kemikali yoyote kwa sababu yametengenezwa na vitu asili. Ukiyapaka mwilini hakuna mbu atakayekusogelea.
Ameeleza kuwa Veta inatoa kozi ya maabara kwa vyuo vinne vya Veta Dar es Salaam, Mtwara, Pwani na Manyara na kwamba lengo la kozi hiyo ni kumuandaa mwanafunzi kuwa mtaalamu wa kuzalisha bidhaa mbalimbali, kupima na kuzingatia ubora na viwango vinavyotakiwa.
Kupitia kozi hiyo tumetengeneza mbolea inayotokana na majani ya maharage kwa ajili ya kilimo na mbolea itokanayo na mazao ya baharini ili kuchochea uchumi wa buluu.” Amesema Issa
Hivyo, amewataka vijana na wahitimu waliomaliza vyuo bila kupata ajira, kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya kusomea fani mbalimbali zitakazowasaidia kujikwamua kimaisha kwa sababu ya ujuzi watakaoupata.
“Tunataka vijana wawe na mawazo bunifu ambayo yatasaidia kutatua changamoto katika jamii hivyo, kuzalisha ajira na kupata kipato kitakachowasaidia kujikwamua kimaisha.”Ameeleza Issa.

Related Posts