‘Wananchi wa pembezoni wasiachwe uboreshaji daftari la kudumu’

Arusha. Viongozi wa dini mkoani Arusha wameisihi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuhakikisha inawafikia wananchi wa maeneo ya pembezoni wakati wa kutoa elimu na kukusanya maoni kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Kwa sasa, INEC imeanza vikao na makundi mbalimbali, ikiwemo viongozi wa dini, wanasiasa na asasi za kiraia, kwa lengo la kutoa elimu na kukusanya maoni kuhusu uboreshaji wa daftari hilo.

Hatua ya kwanza ya kazi hiyo inatarajiwa kuanza Desemba 11 hadi 17 mwaka huu na elimu hiyo inalenga maandalizi ya uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwakani wa madiwani, wabunge na Rais.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Desemba 4, 2024, Sheikh Haruna Hussein, msemaji wa Taasisi ya Kidini ya Kiislamu ya Twariqa Qadiriya Razikia Jailania Tanzania, amepongeza juhudi za INEC katika utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali.

Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuwafikia pia wananchi wa maeneo ya vijijini na pembezoni, ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa sawa ya kushiriki mchakato wa uchaguzi.

“Tunaomba nguvu hii isiishie mijini tu, bali iwafikie hata walioko pembezoni. Lengo ni kuhakikisha kila mtu anaweza kutumia haki yake ya kujiandikisha na hatimaye kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wanaostahili,” amesema Sheikh Haruna.

Ameongeza kuwa viongozi wa dini, mila na wanasiasa wanapaswa kutumia majukwaa yao kuwahamasisha wananchi kujitokeza kuboresha taarifa zao kwenye daftari hilo, ili kuimarisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi.

Kwa upande wake, Mchungaji Yohane Parkipunyi wa Kanisa la Moravian amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao kwenye daftari hilo.

“Ni muhimu kwa wananchi kuhakiki na kuboresha taarifa zao, hasa kwa wale waliobadilisha maeneo ya makazi, waliopoteza vitambulisho vyao vya mpigakura, au vijana waliotimiza miaka 18 karibuni, ili kuhakikisha hawapotezi haki yao ya msingi ya kushiriki uchaguzi,” amesema Mchungaji Yohane.

Related Posts