Wanane mbaroni wakidaiwa kutaka kumteka Tarimo

Dar es Salaam. Siku 23 tangu video za jaribio la kutaka kumteka Deogratius Tarimo, mkazi wa Kiluvya jijini Dar es Salaam zisambae, hatimaye Jeshi la Polisi limesema linawashikilia watuhumiwa wanane wa tukio hilo.

Taarifa ya kushikiliwa kwa watu hao imetolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro leo Jumanne, Desemba 4, 2024.

“Tarehe 11 Novemba, 2024 eneo la Kiluvya, Ubungo Dar es Salaam lilitokea tukio la kutekwa kwa Deogratius Tarimo, mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha mkoani Pwani.

“Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imefanikiwa kukamata kundi la watu wanane wanaotuhumiwa kula njama kwa pamoja na baadaye kufanya tukio la kumteka Deogratius Tarimo. Watuhumiwa wamekamatwa kwa nyakati tofauti Dar es salaam, Songea Ruvuma na eneo la Mbingu Mlimba, Morogoro,”imeeleza taarifa hiyo.

Pia imeongeza kuwa: “lilipatikana gari aina ya Toyota Raum ambayo ilitumiwa wakati wa tukio hilo, huku ikitumia namba isiyo halisi T 237 EGE na baada ufuatiliaji namba halisi ya gari hiyo ni T237 ECF.”

Taarifa hiyo imewataja watuhumiwa hao kuwa ni Bato Bahati Tweve (32), Bondia, mkazi wa Kimara Bunyokwa  na Songwe Mbozi, Yusuph Abdallah (32), mkazi wa Mbingu – Mlimba, Morogoro, Fredrick Juma (31), mkazi wa Kibamba na Nelson Elimusa (24) maarufu msela, dereva teksi, mkazi wa Mbezi Luguluni.

Wengine ni Benk Daniel Mwakalebela (40) maarufu tall, mkazi wa Mbezi -Makabe na Kyela Ipinda, Rusungo Mbeya, Thomas Ephraim Mwakagile (45) maarufu Baba Mage, mkazi wa Bunyokwa na Kyela Ngonga Ndiali- Mbeya, Anitha Alfred Temba (27), mkazi wa Mbezi Mwisho na Isack Mwaifani, maarufu boxer, mkazi wa Kimara Tembo Salanga na Bujonde Isanga Kyela, Mbeya.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linaendelea na kazi ya kuzuia vitendo vya kihalifu pamoja na kuwakamata wote wanaojihusisha na matukio ya uhalifu.

Related Posts