Yanga yaruka mtego wa Waalgeria

HII inaweza kuwa habari njema kwa Yanga baada ya taarifa kutoka Algeria kubainisha kwamba mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi A dhidi ya MC Alger utachezwa palepale ulipopangwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na si vinginevyo.

Awali MC Alger kupitia rais wa klabu hiyo, Mohamed Hakim walipeleka barua CAF kuomba kubadilisha uwanja wa mechi kutoka 5 July 1962 na wakitaka kuutumia Ali la Pointe, lakini ombi lao limekataliwa. Mechi hiyo imepangwa kuchezwa Jumamosi, wiki hii.

Uwanja wa 5 July 1962 uliopo katika Mji wa Algiers ni karibu zaidi na Uwanja wa Ndege wa Houari Boumediene ambao Yanga itatua leo mchana ikitokea Dar es Salaam, hivyo haitawapa wakati mgumu wa kuanzisha safari nyingine kwenda Douera unapopatikana Uwanja wa Ali la Pointe.

Rais huyo wakati akizungumzia ishu ya kutuma ombi la kuhamisha uwanja, alisema: “Barua yetu imepokewa na CAF na upo uwezekano mechi dhidi ya Yanga ikahamishiwa kuchezwa uwanja wetu wa Ali la Pointe. Zipo sababu za msingi sisi kuwasilisha ombi hilo tunataka mechi iwe na mvuto pande zote. Watu wafurahie mpira zaidi.”

Hata hivyo, MC Alger waliangalia mbali zaidi kwani Uwanja wa Ali la Pointe ndiyo wanautumia zaidi kwa mechi za nyumbani za ligi, hivyo wameuzoea zaidi kulinganisha na 5 July 1962.

Kitendo cha CAF kutokubali ombi la wenyeji wa mchezo huo, ni hatua nzuri ambayo Yanga kwao imekuwa nafuu kwani kama mchezo huo ungepelekwa Ali la Pointe, wawakilishi hao wa Tanzania wangelazimika kufanya safari nyingine ya umbali wa kilomita 17.62 kwa gari hadi kufika Douera kutokea Algiers.

“Timu baada ya kuondoka Dar es Salaam

inatarajiwa kufika hapa Algeria kesho (leo Jumatano) majira ya mchana,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye yupo nchini Algeria na kuongeza.

“Baada ya timu kutua hapa Algeria katika Mji wa Algiers, itafikia Hoteli ya Legarcy Luxury ambapo ndiyo kambi itakuwa hapo, ni sehemu tulivu yenye uwezo wa kuwapa wachezaji nafasi nzuri ya kujiandaa na mchezo huo.”

Mtoa taarifa huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kwamba, kitu kizuri ambacho wamefurahia ni kuona mchezo huo utachezwa palepale katika uwanja ambao awali ulipangwa.

“Mwanzoni tulipata taarifa kwamba wapinzani wetu wamepeleka maombi CAF kutaka mechi ihamishwe uwanja ndiyo maana haraka uongozi ukafanya jitihada za kuwatanguliza watu nchini Algeria kufuatilia kwa kina na kama kuna mabadiliko hayo tuone nini cha kufanya.

“Lakini baada ya kufika, imefahamika kwamba mechi itachezwa palepale katika Mji wa Algiers hivyo ni wazi ombi la wenyeji wetu limekataliwa kitu ambacho kwetu kimekuwa nafuu,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mbali na Yanga kuruka mtego huo wa kwanza wa mechi kuhamishwa uwanja, pia nafuu nyingine ipo kutokana na mchezo huo kutokuwa na mashabiki kufuatia maruufu waliyonayo MC Alger.

Hivi karibuni, CAF kupitia kamati yake ya nidhamu, ilitoa hukumu ya kuzuia MC Alger kucheza mechi nne za michuano iliyopo chini ya Shirikisho kufuatia matendo yao ya kinidhamu yaliyofanywa katika mchezo wa mwisho wa kufuzu hatua ya makundi msimu huu waliposhinda nyumbani 2-0 dhidi ya US Monastir.

Yanga huu utakuwa ni mchezo wa pili wa Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ule wa kwanza nyumbani kufungwa 2-0 na Al Hilal. MC Alger kwao pia ni wa pili kufuatia ugenini kupata matokeo ya 0-0 dhidi ya TP Mazembe.

Kufuatia Yanga kuuchukulia mchezo huo kwa umakini mkubwa kama ilivyon kwa wenyeji wao, Kocha Mkuu, Sead Ramovic amesema kuna kitu ameanza kukiona kikosini kwake.

Ramovic ambaye tangu atambulishwe kikosini hapo Novemba 15 mwaka huu na kuiongoza Yanga kucheza mechi mbili za kimashindnao ikiwemo moja Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine Ligi Kuu Bara, amesema wachezaji wake wameanza kuingia kwenye falsafa anayoitaka.

Wikiendi iliyopita baada ya Yanga kupata ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, Ramovic amesema: “Ingawa tumefunga mabao mawili dhidi ya Namungo lakini bado kuna ishu ya kutumia nafasi haijakaa sawa, nataka kuona wachezaji wakitumia vizuri nafasi tunazotengeneza ili kufunga mabao mengi.

“Ninaamini nina safu bora ya ushambuliaji inayohitaji marekebisho kadhaa ikiwemo kujengwa kisaikolojia ili kurudisha ufanisi wake.”

Ukiangalia kikosi cha Yanga, washambuliaji wao wanne wamekuwa na mchango mdogo wa mabao hasa ligi ya ndani.

Katika washambuliaji hao, Clement Mzize na Kennedy Musonda ndio kidogo wana mchango mkubwa wa mabao kulinganisha na Prince Dube na Jean Baleke.

Baleke ambaye amecheza mechi nne za ligi msimu huu kwa dakika 166, amefunga bao moja, hana asisti wakati Prince Dube akicheza mechi 10 kati ya 11 kwa dakika 446 bila ya bao akiwa na asisti moja.

Kwa upande wa Mzize, amefunga mabao matatu katika mechi 10 akicheza kwa dakika 457, hana asisti huku Musonda aliyekiwasha katika mechi za kufuzu Afcon 2025 akiwa na Zambia akifunga mabao matano, ndani ya Yanga msimu huu kwenye ligi amefunga mabao mawili, hana asisti akicheza mechi nane kwa dakika 232.

Jana mchana, Yanga ilianza safari kwenda Algeria ikiwa na msafara wenye watu 53 wakiwemo wachezaji 25.

Wachezaji waliosafiri ni makipa; Djigui Diarra, Aboutwalib Mshery na Khomein Abubakar.

Mabeki: Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Abdullah, Kouassi Yao Attohoula, Nickson Kibabage,  Kibwana Shomari na Chadrack Boka.

Viungo: Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya, Khalid Aucho, Stephane Aziz Ki, Denis Nkane, Sheikhan Khamis, Duke Abuya, Clatous Chama, Jonas Mkude na Farid Mussa.

Washambuliaji: Kennedy Musonda, Clement Mzize, Prince Dube na Jean Baleke.

Related Posts