Afrika yatakiwa kuwekeza kwenye ubora wa rasilimali watu

Dar es Salaam. Wakati nchi za Afrika zikijivunia kuwa na wingi wa rasilimali ikiwemo ardhi, gesi, mafuta na madini, imeelezwa kuwa endapo hautafanyika uwekezaji wa rasilimali watu katika kuziendeleza rasilimali hizo hazitakuwa baraka kama ambavyo tayari imeanza kuonekana katika mataifa mbalimbali ya bara hilo.

Kukabiliana na hilo nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo zimetakiwa kuwekeza katika rasilimali watu ili kuwaandaa vyema katika kuzichakata na kuziendeleza rasilimali hizo kinyume na hilo zitaishia kuleta balaa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameyasema hayo leo wakati akifunga kongamano la tisa la sayansi, teknolojia na ubunifu lililoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Profesa Mkenda ambaye ni mbobezi wa uchumi amesema licha ya kuwepo kwa nadharia mbalimbali kuhusu maendeleo ukweli ni kwamba ubora wa rasilimali watu ndiyo unaoweza kuleta maendeleo katika nchi.

Amesema kwa kutambua hilo Tanzania imeanza kuongeza uwekezaji kwenye elimu hasa katika sayansi na teknolojia ili kutengeneza rasilimali itakayoweza kuzichakata na kuziendeleza rasilimali zilizopo.

 “Nchi nyingi za Afrika rasilimali zimekuwa siyo baraka kwao bali ni balaa na hii ni kwa sababu ya kutofanyika uwekezaji wa kutosha kwenye rasilimali watu, matokeo yake kunakuwa na utegemezi mkubwa wa watu kutoka mataifa nyingine.

 “Hili tunaendelea kulifanyia kazi kwa kuhakikisha tunafanya uwekezaji mkubwa kwenye elimu hasa sayansi na teknolojia ili vijana wetu wabobee kwenye sayansi, teknolojia na ubunifu na ndiyo sababu tumeanzisha mfumo maalumu kwa ajili ya kuendeleza kazi za ubunifu,” amesema Profesa Mkenda.

Kupitia mfuko huo Waziri Mkenda amesema wabunifu sasa watawezeshwa kuendeleza bunifu zao hasa zile zinazotatua changamoto zilizopo kwenye jamii kwa kufikishwa katika kiwango cha kupelekwa sokoni.

Amesema, “Kila mwaka kwenye maonesho tunaona bunifu mbalimbali lakini haziendelezwi, sasa ifike mwisho ni lazima tuwe uendelezaji wa hizi kazi zikawe msaada kwenye jamii.”

bali na hilo Profesa Mkenda amesema kuanzia sasa Serikali kupitia wizara hiyo itaanza kuwaangalia kwa ukaribu watafiti ili tafiti wanazofanya zisiishie kwenye makabati, ni lazima zikafanyiwe kazi kukamilisha lengo la utafiti husika,” amesema Profesa Mkenda.

 Akizungumzia hilo mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge elimu, utamaduni na michezo Husna Shekiboko amesema kuna tatizo kubwa la tafiti zinazofanywa na wataalamu kutofanyiwa kazi. “Kuna udhaifu mkubwa kwenye kuzifanyia kazi tafiti zinazofanywa na hawa wenzetu wataalamu, hawa wanafanya tafiti, wanaandika maandiko na kutoa ushauri lakini sisi watekelezaji tunaweka kabatini.

 “Kupitia kongamano hili naahidi Bunge litasimamia kikamilifu kuhakikisha yale yote ambayo yanachakatwa na wasomi kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii na zile zinazolenga kuleta maendeleo yanafanyiwa kazi mawazo yao,”amesema Husna.

Mkurugenzi wa Costech, Dk Amos Nungu amesema kupitia kongamano hilo masuala mbalimbali yamejadiliwa ikiwemo kuwezesha usambazaji na matumizi ya bidhaa za utafiti na ubunifu.

Lingine ni kuhamasisha kizazi kijacho cha wavumbuzi wa kazi za ubunifu, teknolojia na sayansi kwa kutoa msukumo kwa vijana na wanafunzi katika shule za msingi na sekondari kupenda masomo ya sayansi.

Related Posts