AKILI ZA KIJIWENI: Kijiwe kimembariki Yondani Pamba

IWE ni umri sahihi au sio sahihi, wote tunakubaliana kwamba Kelvin Yondani ‘Vidic’ ni mtu mzima hasa kwenye Ligi yetu ya Tanzania Bara ukilinganisha na mabeki wengi wa kati.

Nyaraka zake mbalimbali zinaonyesha kuwa alizaliwa Oktoba 4, 1984 hivyo kwa sasa tayari ametimiza miaka 40 hivyo kiuhalisia wachezaji wengi wa Ligi Kuu ni wadogo zake na wengine ni kama watoto wake maana wapo waliozaliwa wakati Anko Yondani ameshaanza kucheza Ligi Kuu.

Sasa baada ya kukaa nje ya uwanja bila timu tangu alipoachana na Geita Gold iliposhuka daraja mwishoni mwa msimu uliopita, jamaa mara tu dirisha dogo la usajili msimu huu litakapofunguliwa tutamuona akiwa katika jezi za Pamba Jiji FC.

Mabao ambayo Pamba imekuwa inaruhusu yameushtua uongozi wa timu hiyo na kuona unahitajika kuimarisha ukuta wake na katika mpango huo imemuona Yondani kama mtu sahihi wa kuipa uimara safu yake ya ulinzi ambayo hadi muda huu tunaizungumzia hapa kijiweni, tayari imeshafungwa mabao 14 katika mechi 13.

Sio kwamba Pamba haijawaona mabeki vijana au kwenye kikosi chake hawapo lakini hadi inaamua kumsajili Yondani maana yake inaamini kuna kitu kikubwa atakiongeza kikosini ambacho kinakosekana hivi sasa.

Yondani ataipa safu ya ulinzi ya Pamba utulivu lakini pia uongozi kwa vile hadi sasa inamkosa mchezaji ambaye ana hizo sifa na pia uzoefu wake utakuwa na faida kubwa katika kuwakomaza kiakili mabeki wengine.

Kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, Yondani ni mtu anayehitajika kuwajengea wachezaji vijana hali ya kujiamini lakini pia kuwashusha presha pale mambo yanapoonekana kuwa magumu klabuni hasa muda ambao timu itapata matokeo yasiyo mazuri.

Usajili wa Yondani ndani ya Pamba unaendelea kudhihirisha kuwa umri ni namba tu ambazo sio za kuzizingatia sana kwenye soka bali kinachotakiwa kutazamwa ni ufanisi wa mchezaji husika kama una faida au hauna kwa timu anayochezea.

Vijana wamepewa fursa wanashindwa kuitumia ndio maana hapa kijiweni tumeamua kumfagilia Kelvin Yondani kwa sababu kile anachokifanya kinaonekana kukosekana mtu wa kukirithi.

Related Posts