KESHOKUTWA kuanzia saa 4:00 usiku tutakuwa bize hapa kijiweni tukitazama mechi ya wawakilishi wetu wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga dhidi ya MC Alger itakayochezwa jijini Algiers, Algeria.
Dua zetu zitakuwa kwa Yanga ipate ushindi katika mechi hiyo kwani ndio matokeo yatakayoweka hai matumaini yake ya kuingia robo fainali baada ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Al Hilal katika kundi lake A kwa mabao 2-0.
Na kwa vile kisasi ni haki, Yanga inatakiwa kushinda mechi hiyo ili kulipa kisasi cha kufungwa mabao 4-0 katika mechi yake ya mwisho ambayo ilicheza nchini Algeria dhidi ya MC Alger mwaka 2017. Sisi hapa maskani tuna kumbukumbu sana ya matokeo yale.
Baada ya mechi hiyo ya Yanga, keshokutwa yake huko huko Algeria lakini kwenye mji wa Constantine, kutakuwa na mechi nyingine ya wawakilishi wengine wa Tanzania lakini kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Simba dhidi ya CS Constantine ya huko ambayo itachezwa kuanzia saa 4:00 usiku pia.
Simba yenyewe angalau inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Onze Bravos ya Angola katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi wiki iliyopita.
Kama ilivyo kwa Yanga, Simba nayo inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi ya mwisho ambayo ilicheza Algeria ambako ilichapwa mabao 2-0 na JS Saoura mwaka 2019.
Hata hivyo, historia hizo hazitakiwi kuzitisha Yanga na Simba badala yake izipe changamoto na ari ya kujiandaa vizuri na kupambana zaidi ndani ya dakika 90 za mchezo ili kila moja ipate pointi tatu muhimu ambazo zitaiweka kwenye nafasi nzuri katika kundi lake.
Timu hizo mbili zinazoiwakilisha Tanzania kwa sasa zimebadilika sana kulinganisha na mara ya mwisho zilipopoteza mechi huko Algeria na kiukweli zina uzoefu wa kutosha na wachezaji wazuri ambao wanaweza kucheza mechi dhidi ya timu ngumu na bora na kupata matokeo mazuri iwe nyumbani au ugenini.
Hazitakiwi kuingia kinyonge kwenye mechi hizi za raundi ya pili ya hatua ya makundi na zikaze hasa ili zilete furaha na heshima hapa Tanzania huku zenyewe zikijiweka pazuri katika makundi yao.