Algeria kumechangamka, Benchikha auza faili Yanga

YANGA wameshatua Algeria kwa ajili ya mchezo wa pili wa kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwafuata wenyeji wao, MC Alger ambao wanakutana Jumamosi, wiki hii jijini Algiers.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wameondoka nchini wakitoka kushinda mchezo wa ligi dhidi ya Namungo, ikiwa ni baada ya kupoteza michezo miwili ya mashindano hayo na mmoja wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal.

Hata hivyo, baada ya juzi kupangua mtego wa awali wa uwanja wataoutumia kuchezea mchezo huo wa ugenini dhidi ya MC Alger ambao wamekataliwa kubadilisha uwanja na Shirikisho la Soka Afrika, habari njema ni kwamba mambo ya watetezi hao wa ligi yanaendelea kuwa mazuri huko ugenini.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdelhak Benchikha amewauzia faili Yanga dhidi ya MC Alger kuelekea mchezo huo ambao utachezwa bila ya mashabiki, Benchikha amewaambia Yanga wanapaswa kuwa makini sana na mashambulizi ya kushtukiza ambayo MC Alger wamekuwa wakiyatumia zaidi.

MC Alger watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaochezwa Jumamosi wiki hii saa 4 usiku kwenye Uwanja wa 5 July 1962 uliopo Algiers nchini Algeria.

Mulgeria huyo ambaye kwa sasa anainoa JS Kabylie inayoshika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Algeria huku MC Alger ikiwa ya pili, amesema kwa anavyoifahamu Yanga, anaipa nafasi kubwa ya kufanya vizuri lakini lazima ifanye kazi ya ziada.

Kocha huyo aliyeifundisha Simba kuanzia Desemba 2, 2023 hadi Aprili 29, 2024, alisema ameiona Yanga ni timu yenye kikosi kizuri lakini hivi karibuni imekuwa na tatizo katika kuruhusu mabao kwa mashambulizi ya kushtukiza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Benchikha alisema ukiachana na mfumo wa ushambuliaji wa MC Alger, lakini kitendo cha kufungiwa mashabiki wake pia ni hatua kubwa ya Yanga kufanya vizuri kwenye mechi hiyo.

Alisema kuwa, MC Alger mashabiki wake wamekuwa na nguvu ya kuisaidia timu yao kupata ushindi kutokana na namna wanavyotoa presha kwa wapinzani pindi wanaposhangilia.

“MC Alger inacheza soka la mashambulizi ya kushtukiza, Yanga wanatakiwa kujipanga sana na hilo kwani ushindi wao umekuwa ukitokana na mashambulizi ya aina hiyo,” alifichua kocha huyo.

“Naijua Yanga inayoundwa na wachezaji wazoefu, naamini haitakuwa rahisi kwa wenyeji wao, nilikutana na Yanga kwenye Fainali ya Shirikisho nikashinda lakini kazi kubwa tulifanya,” alisema Benchikha ambaye aliiongoza USM Alger kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-23 ikicheza fainali dhidi ya Yanga iliyokuwa ikinolewa na Nasreddine Nabi. Mechi ya kwanza Dar, USM Alger ilishinda 2-1, kwao ikafungwa 1-0 na kubeba ubingwa kwa faida ya bao la ugenini.

Kocha huyo alibainisha kwamba, mbali na kuifahamu Yanga pindi akiwa USM Alger, lakini alikutana nayo katika Ligi Kuu Bara wakati akiifundisha Simba na kupoteza kwa mabao 2-1.

“Yanga pia nikaja kukutana nayo nikiwa na Simba, wakanifunga, naelewa kuwa timu hiyo sio rahisi kukubali kupoteza ikiwa ugenini kwani iko makini sana linapokuja suala la mechi za kimataifa,” alisema kocha huyo anayeifundisha JS Kabylie ya Algeria.

Wakati Benchikha akisema hayo, rekodi zinaonyesha kwamba Yanga imekuwa na matokeo mazuri ikicheza uwanja wa ugenini msimu huu tofauti na wapinzani wao wakiwa kwao nyumbani.

Katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga imecheza michezo 11 na sita kati ya hiyo ni ya ugenini, ambapo imeshinda yote kwa maana imekusanya pointi 18, huku ikiwa imefunga mabao manane, haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.

Kwa upande wa michezo ya nyumbani, Yanga imecheza mitano, kati ya hiyo imeshinda mitatu na kupoteza miwili ikiwa na pointi tisa, imefunga mabao manane na kuruhusu manne. Kwa jumla, timu hiyo imekusanya pointi 27 ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

MC Alger katika Ligi ya Algeria ‘Ligue 1’, imecheza michezo 10 na mitano kati ya hiyo ni nyumbani, ambapo rekodi zinaonyesha imeshinda mmoja, sare mitatu na kupoteza mmoja, ikiwa imefunga mabao matatu na kuruhusu manne.

Timu hiyo anayoichezea aliyekuwa nyota wa Azam FC, Kipre Junior, kwa michezo ya ugenini imecheza mitano, ikishinda mitatu na kutoka sare miwili ambapo imefunga mabao matano tu na kuruhusu mawili, ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi yao na pointi 17.

Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic alisema mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara ambao timu hiyo ilishinda mabao 2-0, ugenini dhidi ya Namungo kwa kiasi kikubwa uliamsha ari ya wachezaji, baada ya kuanza vibaya mechi yake ya kwanza kwa kufungwa 2-0 dhidi ya Al Hilal ukiwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Kila mmoja wetu yupo katika hali nzuri ya kupigania pointi ngumu za kwanza ugenini, utakuwa mchezo wa tofauti kabisa kwa sababu tunahitaji kurejesha morali kwa mashabiki zetu na kuweka matumaini ya kundi letu hai,” alisema na kuongeza:

“Tunahitaji kufanya vizuri zaidi ya tulivyoanza, kuhakikisha hatuwapi nafasi ambazo zinaweza kutugharimu huku tukicheza kwa lengo la kupata pointi tatu ugenini, kama nilivyosema hapo awali kwamba ni mchezo mgumu ila kila kitu kinawezekana.” 

Katika kundi A, Al Hilal inaongoza ikiwa na pointi 3, inafuatiwa na MC Alger (1) sawa na TP Mazembe (1) huku Yanga ikiwa na 0.

Related Posts