Katavi. Askari wawili wa Hifadhi ya Taifa (Tanapa) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumshambulia kwa risasi hadi kumuua Gimbagu Lengu Mandagu (25) mfugaji na mkazi wa Kijiji cha Ikuba Wilaya ya Mlele mkoani katavi.
Joseph Malawa ambaye ni shuhuda wa tukio la mauaji ya mfugaji huyo lililofanywa na askari wa hifadhi Tanapa, anaeleza kuwa aliowaona askari hao wakimpiga risasi mfugaji huyo.
“Ilikuwa mchana nikiwa shamba yule mfugaji alikuwa anachunga ng’ombe pembezoni mwa shamba langu ghafla nikaona askari wanakuja wanakimbia yule mfugaji alivyowaona alianza kukimbia ndipo wakaanza kumimina risasi.
Kijana huyo (marehemu) hakusimama aliendelea kukimbia, Alikimbia umbali akamaliza mashamba kama manne hivi ndipo wale askari wakafyatua risasi iliyomuangusha chini yule mfugaji.
Amesema baada ya tukio hilo askari hao wakaanza kuwafukuza watu waliokuwa mashambani wakiwataka kuondoka agizo ambalo walilitekeleza.
“Hata hivyo hatukwenda mbali tukaona gari imekuja na kuwachukua wale askari na mwili wa marehemu wakaondoka nao tulivyofika alipokuwa ameuliwa tulikuta damu nyingi zimefukiwa na askari na fimbo ya marehemu imeachwa pembeni,”
Michael Malubwa ambaye ni shuhuda mwingine wa tukio hilo amesema matukio ya askari wa hifadhi kuvamia na kuua watu katika maeneo yao yamekuwa yakijirudia mara kwa mara kwani ni tukio la tatu watu kupoteza maisha kwa kuuawa na askari wa Tanapa huku wakitoa fedha kwenye misiba ya watu ambao wamewaua.
“Wanaingilia wananchi kwa kusogeza mipaka kwenye mashamba na makazi ya watu, jambo ambalo linafanya watu tushindwe kuishi kwa amani na utulivu katika maeneo yetu ya asili tumelalamika sana lakini hatua hazichukuliwi na serikali sasa sisi tufanyaje’’ alihoji Malubwa,
Maduka Mandalu ambaye ni kaka wa marehemu amesema,”Matukio haya yanaongozwa na viongozi wa juu katika wilaya na mkoa kwani wao ndio wanaanzisha operesheni hizi na kila tukilalamika hawachukui hatua tunaomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie kutatua matatizo yetu.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 5, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo askari wawili wa Hifadhi ya Taifa Tanapa wanashikiliwa kwa kosa la kumshambulia kwa risasi mfugaji na kusababisha kifo chake.
Ngonyani amesema tukio hilo limetokea Desemba 3, 2024 mwaka huu katika Kitongoji cha Ipota kilichopo Kata ya Ikuba wilayani Mlele ambapo askari wa Tanapa walikuwa katika dori ya kawaida katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii (WMA) Ikuba wakifuatilia ng’ombe ambazo zilikuwa zinachungwa katika pori hilo.
Ameeleza kuwa baada ya kuwakuta ng’ombe hizo zikichungwa kwenye hifadhi ya pori la jamii ndipo wafugaji waliwazingira askari wa Tanapa wakitaka kuwashambulia ndipo askari wa Tanapa wakaanza kurusha risasi angani ili kuwatawanya na risasi moja ikampata mfugaji mmoja aliyejulikana kwa jina la Gimbagu Lenga Mandagu.
‘’Kweli tukio hili limetokea na tunawashikilia askari wawili wa Tanapa wanaodaiwa kumshambulia mfugaji, lakini niwaombe wananchi hasa wafugaji kujiepusha na kuingiza mifugo kwenye hifadhi na badala yake wanatakiwa wafuate sheria na taratibu za kulisha mifugo yao katika maeneo ambayo yanaruhusiwa kisheria,’’amesema Ngonyani.